Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam mheshimiwa Albert Chalamila amezindua kampeni ya utoaji wa huduma za afya bure(Afya check) mkoa wa Dar es salaam na kuwataka wananchi kuheshimu taaluma ya udaktari.
Akiwa katika uzinduzi wa kampeni hiyo kimkoa iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya msingi Mbagala Rangitatu, Mhe. Chalamila amewaasa wananchi kutokuchezea kada hiyo kwa kuwa inagusa moja kwa moja uhai wa binadamu.
Mkuu huyo wa Mkoa amegusia kipande cha video fupi kilichosambaa mitandaoni kikimuonesha mmoja wa wauguzi akisafisha vifaa vya hospitali na kuvianika juani na kusema kitendo hicho si sawa lakini pia si sahihi kumuona mwenzako akipata matatizo kazini.
“Tusifurahie sana mimi mkuu wa Mkoa nikaja hapa nifanye maamuzi kuwa daktari huyu aondoke,itafika kipindi mtoto wako ataumwa na mimi sio daktari,mtoto wako atakufa…ukiona kuna mtumishi wa afya amekosea,fuata viongozi waeleze watakaa nae waongee ikishindikana mwisho ndio ifike hatua ya kufukuzana”.Alisema Mkuu huyo wa Mkoa
Kampeni hiyo ya utoaji wa huduma Bure za afya ulioratibiwa na wadau mbalimbali wakiwemo kipindi cha Afya Check kinachoongozwa na Dkt Isaac Maro,imezinduliwa kimkoa leo ambapo jumla ya watu elfu 20 wanatarajiwa kupatiwa matibabu na vipimo vya afya bure katika mkoa huu wa Dar es salaam.