
Baba Askofu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki, Askofu Lawi Mwankuga, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki kupiga kura Oktoba 29, 2025, huku wakitanguliza amani na umoja wa kitaifa kama msingi wa maendeleo endelevu ya nchi.
Akizungumza Oktoba 28, 2025 jijini Dar es Salaam, mara baada ya vyama vya siasa kumaliza kampeni zao za Uchaguzi Mkuu, Askofu Mwankuga amekumbusha kuwa uchaguzi ni tukio la muda mfupi, lakini maisha na ustawi wa taifa vinaendelea hata baada yake, hivyo Watanzania wanapaswa kudumisha upendo na mshikamano.
Aidha, amewataka wanasiasa wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi kuzingatia maslahi ya wananchi na kuishi ahadi walizotoa wakati wa kampeni, endapo watapewa ridhaa ya kuongoza kupitia sanduku la kura.
Askofu Mwankuga amesisitiza pia umuhimu wa kuchagua viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi, bila kujali vyama vyao, katika nafasi za Udiwani, Ubunge na Urais, akisema maendeleo ya taifa hayapaswi kuwa na mipaka ya itikadi za kisiasa.
Vilevile, amewapongeza Watanzania kwa mwitikio mkubwa wa kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura, akisisitiza kuwa ni wajibu wa mamlaka kuheshimu maamuzi ya wananchi watakapokuwa wamechagua viongozi wanaowataka.
“Ni muhimu mamlaka zikaheshimu matokeo ya kura kama ishara ya demokrasia na heshima kwa sauti ya wananchi, kwani hilo ndilo chimbuko la amani na utulivu wa taifa letu,” amesema Askofu Mwankuga.
