
Kesi mbili zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, zinatarajiwa kunguruma tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakati kesi ya uhaini ikipangwa leo Jumanne Julai 15, 2025 kwa ajili ya kutajwa na Serikali kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo nayo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
Lissu anakabiliwa na kesi hiyo pamoja na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni, mahakamani hapo.
Julai Mosi 2025, upande wa mashtaka uliomba upewe muda zaidi wa kutoa uamuzi wa hatima ya kesi ya uhaini baada ya upelelezi kukamilika na jalada la kesi kupelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya kusomwa na kutolewa uamuzi.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Franco Kiswaga, anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka.