Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango imekamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, nyaraka kuu ya kisera inayotarajiwa kuongoza mikakati ya maendeleo ya muda mrefu kwa miongo ijayo. Dira hiyo itazinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, katika hafla maalum jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 15, 2025, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa maandalizi ya Dira hiyo yamefanyika kwa kipindi cha takriban miaka miwili, yakijikita katika ushirikishwaji mpana wa jamii na makundi mbalimbali ya kitaifa.
“Kupitia zoezi hili, tumepokea maoni kutoka kwa zaidi ya Watanzania milioni 1.174 waliotoa maoni yao kwa njia mbalimbali, na zaidi ya wananchi 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa kujadili mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Dkt. Msemwa.
Alisema kuwa katika hatua za awali, Tume ilifanya uchambuzi wa nchi zilizopiga hatua katika maendeleo ya uchumi wa kati, kwa lengo la kujifunza mikakati yao na kuchukua maarifa muhimu ya kuijenga Tanzania mpya ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Msemwa alibainisha kuwa baada ya kuandaliwa, rasimu ya Dira ya 2050 ilirudishwa kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa maoni yao yamezingatiwa kikamilifu kabla ya kuipitisha rasmi. Pia, nyaraka hiyo imewasilishwa kwa wadau wa sekta binafsi, asasi za kiraia, wawakilishi wa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu pamoja na taasisi za elimu ya juu ili kujenga umiliki mpana wa Taifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa, utekelezaji wa Dira mpya utaanza rasmi mwezi Julai 2026, mara baada ya kumalizika kwa Dira ya sasa ya Maendeleo ya 2025 ambayo imekuwa muongozo wa maendeleo kwa kipindi cha takriban miaka 25.
Tume ya Taifa ya Mipango ina jukumu la kuratibu maandalizi na utekelezaji wa mikakati ya kitaifa ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa malengo ya muda mrefu yanazingatia misingi ya ushirikishwaji, ujumuishi, na uendelevu wa maendeleo kwa Watanzania wote.
Dira ya Maendeleo ya 2050 inatarajiwa kuweka mwelekeo wa wazi kuhusu vipaumbele vya Taifa katika maeneo kama uchumi wa viwanda, maendeleo ya watu, mabadiliko ya teknolojia, mazingira, na usawa wa kijinsia – yote yakiwa yamejengwa juu ya msingi wa mshikamano wa kitaifa.