Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amesikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata za Mwataga, Kishapu na Uchunga katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 25, 2025 katika maeneo hayo.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni huduma ya maji safi, upatikanaji wa umeme, uboreshaji wa barabara,uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano ya simu Uchunga, huduma za afya katika Zahanati ya Lubaga na ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Lubaga.
“Ndugu zangu wananchi niwapongeze kwa kuendelea kuiamni serikali ya awamu ya sita na pia napenda kuhamasisha kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuepuka mikusanyiko isiyo na tija na kuwekeza zaidi katika familia zenu hususa ni katika maendeleo ya wanawake na watoto” amesema Masindi
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wazazi kuwasomesha watoto wao na kuwaendeleza kwenye vipaji mbalimbali waliofeli masomo huku wakiwawekeza zaidi kwenye malezi bora yenye kufuata maadili ya KiTanzania huku akiahidi mahitaji mengine ambayo hayapata utatuzi serikali inaendeleza jitihada ya kuzitatua kwa haraka ili wananchi wanufaike na nchi yao.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu, David Mashauri,akijibu maswali ya sekta ya elimu amesema Halmashauri imeanza kupokea fedha kwa ajili ya kujenga Shule shikizi katika maeneo yenye changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu huku Kitongoji cha Lubaga kilichoko Kata ya kishapu kikiwa ni miongoni wa wanufaika.
Mashauri ameongeza kuwa Shule ya Msingi Bukingwa-Mandenge na Bulima tayari zimepangiwa fedha kwa ujenzi wa madarasa, huku nyumba ya Walimu Shule ya Msingi Lubaga ikiwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 wanasubiria fedha ili kuboresha jengo hilo.
Meneja wa RUWASA Wilayani humo, Dickson Kamazima, amesema serikali inaendelea kusogeza huduma ya maji safi kwa wananchi ambapo kwa Kitongoji cha Mwataga utekelezaji umefikia asilimia 95, na maeneo mengine yatapatiwa huduma kupitia maji ya Ziwa Viktoria na visima vinavyochimbwa kisasa.
Aidha amesema wiki ya kwanza ya Septemba watafanya uthamini katika Kitongoji cha Migunga ili kusogeza huduma hiyo kupitia kwenye bomba kubwa la maji linaloelekea Kata ya Lagana, huku Kitongoji cha Mwanulu kikiwa kwenye mpango wa kusogezewa huduma pia baada ya kupokea fedha kutoka serikalini.
Kwa upande wa umeme, Mwakilishi wa Meneja wa TANESCO Wilayani humo, Gidion Kanan, amesema serikali inaendelea kusambaza nishati hiyo kwenye Vijiji na vitongoji kote Wilayani humo.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya umeme na kuunga mkono matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira.
Wananchi wameendelea kuzipongeza jitihada za serikali kwa kusogeza huduma muhimu za kijamii jambo linalosaidia kujenga jamii bora na yenye matumaini imara.