Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kilimani, Jimbo la Dodoma Mjini, wamehimizwa kuvunja makundi yote yaliyokuwa yamejitokeza wakati wa mchakato wa kuwania nafasi ya udiwani ili kujenga mshikamano kuelekea ushindi wa chama katika uchaguzi ujao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilimani, Comrade Nathan Chibeye, wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama uliofanyika kwa ajili ya kuwajulisha wanachama kuhusu mgombea mteule wa nafasi ya udiwani na kuweka mikakati ya kuanza kampeni rasmi.
“Niwaambie ndugu zangu, mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama chetu umekwisha,tuliokuwa watia nia tumejitokeza tisa, lakini ilibidi mmoja ateuliwe.
Vikao halali vya chama vimemteua Mhe. Mussa Elias Mkunda kuwa mgombea wetu hivyo, makundi yote sasa yafutwe tubaki na kundi moja tu la CCM Msimkomeshe aliyechaguliwa na chama, mkumbuke kuna maisha baada ya uchaguzi,” amesema Comrade Chibeye.
Mkutano huo maalum ulikuwa na ajenda kuu mbili: kuvunja makundi na kuanza maandalizi ya kampeni kwa ajili ya kumnadi mgombea udiwani wa CCM katika kata hiyo.
Wakati wa mkutano huo, watia nia wote tisa walipewa nafasi ya kutoa maoni na kushauri kuhusu hatua ya mbele ya chama. Rotta Ndimbo, Katibu Mstaafu wa CCM Kata ya Kilimani na mmoja wa waliotia nia, alisisitiza umuhimu wa mshikamano baada ya mchakato.
“Ndugu zangu, mimi nilikuwa na kundi langu. Lakini sasa uchaguzi wa ndani umekwisha. Sote tunarudi kuwa kundi la CCM. Mgombea wetu ni Mhe. Mussa Elias Mkunda. Tuungane kuhakikisha Oktoba 29 tunashinda kwa kishindo kwa kura za kutosha kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu Paskali Chinyele, na Diwani wetu mteule,” alisema Ndimbo.
Mhe. Neema Mwaluko, Diwani Mstaafu wa Kata ya Kilimani, alisisitiza umuhimu wa kampeni za kisayansi na kuonyesha utayari wake katika kusaidia chama kufanikisha ushindi.
“Sasa tumeshapata mgombea. Tuhakikishe tunafanya kampeni za nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda, hadi shuka kwa shuka. Niko tayari kwa mapambano kuhakikisha Oktoba 29 ni ushindi kwa CCM,” alisema Mhe. Mwaluko.
Mhe. Mussa Elias Mkunda, mgombea mteule wa CCM, aliwashukuru waliotia nia na kuahidi kuwa kiongozi anayeshirikiana na kila mmoja bila ubaguzi. Alieleza kuwa anaheshimu mchango wa viongozi waliomtangulia na anaahidi kushirikiana nao.
“Si mimi bora sana kuliko wenzangu; bali Mwenyezi Mungu alitenda. Nitakuwa kiongozi wa ushirikiano, nitasikiliza na kufungua milango kwa kila mmoja. Nitahakikisha tunaboresha huduma za miundombinu, elimu, afya, pamoja na kuinua uchumi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na halmashauri,” alisema Mkunda.
Katika kumaliza kikao hicho, wanachama walisisitiza kauli mbiu yao kuwa ni “Kazi na Utu – Tusonge Mbele.” Wote walikubaliana kuwa Oktoba 29 iwe siku ya ushindi wa tikiti tatu:
Chama cha Mapinduzi Kata ya Kilimani sasa kinaelekea kwenye hatua ya kampeni kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya — kwa Umoja na Ushindi wa CCM!