Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amewakabidhi wakulima wanne Wilayani humo matrekta yenye thamani ya Shilingi 238,400,000/=, yaliyopatikana kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya NMB.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Septemba 25, 2025, katika viwanja vya Benki ya NMB Wilayani humo Masindi amesema hatua hiyo ni chachu ya kuwaletea wamiliki wa matrekta hayo ongezeko la kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa.
Benki ya NMB Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Alexander Macheko akizungumza wakati Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi akikabidhi Kwa wakulima wanne matrekita yenye thamani ya Tsh. 238,400,000 Kwa mkopo kutoka Banki ya NMB Wilayani humo Septemba 25,2025
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia NMB imetoa mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 9. Tuyatumie kwa malengo ya kuongeza kipato cha familia huku mkikumbuka kurejesha mikopo hiyo kwa mujibu wa mkataba,” amesema Masindi.
Ameongeza kuwa serikali ya Awamu ya Sita inatambua thamani ya mkulima kwa kuwa sekta ya kilimo ni mhimili wa pato la taifa, na hivyo wamiliki wa matrekta wanapaswa kuwa mfano wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia badala ya kilimo cha jembe la mkono na kutumia mifugo.
Aidha, amewataka wamiliki wa matrekta hayo kuwashirikisha vijana kwa kuwaelezea faida za kilimo cha kisasa kupitia zana hiyo ili nao watumie fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.
“Vijijini mnakokaa tangazeni huduma za kulima kwa trekta. Wakulima watawafuata, ninyi mtaongeza kipato, familia zenu zitapata nafuu na marejesho ya mkopo hayatakuwa kikwazo,” amesisitiza
Kwa upande wake, Meneja wa Banki ya NMB Wilayani humo Alexander Gabriel Macheko, amesema lengo la kutoa mikopo hiyo ni kusaidia kuinua sekta ya kilimo na kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
“Tunaamini wamiliki hawa wanne watahamasisha jamii zao kuhusu urahisi na faida ya kutumia trekta. NMB pia inatoa mikopo kwa wafugaji wanao nenepesha mifugo, wajasiriamali wadogo ili kuinua biashara zao na watumishi wapya ambao hawajathibitishwa kazini, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema Macheko.
Nao wakulima walionufaika na mkopo huo akiwemo Sagala Luminu, Magida Luahu, Saba Kwihula na Machiya Mhuli, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua mchango wa wakulima, wakibainisha kuwa mikopo hiyo yenye masharti nafuu itawaondolea changamoto ya muda mwingi ambapo awali walikuwa wakitumia jembe la mikono na mifugo kama Punda na Ng’ombe na sasa itawasaidia kuongeza tija kwenye kilimo.