
Mahusiano kati ya Ethiopia na Sudan yameendelea kuzorota baada ya nchi hizo mbili kufunga balozi zao ndogo zilizoko karibu na mpaka wao wa pamoja na kuwafukuza wanadiplomasia waliokuwa wakifanya kazi maeneo hayo.
Sudan inaishutumu Ethiopia kwa kuwaunga mkono waasi wa RSF wanaopigana na jeshi la Sudan, huku Ethiopia ikiituhumu Sudan kwa kuwaunga mkono waasi wa Tigray wa TPLF.
Pande zote mbili zimekuwa zikikanusha tuhuma hizo.
Wiki hii Sudan pia iliwasilisha malalamiko katika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika dhidi ya Ethiopia.
Hatua hiyo inaongeza wasiwasi wa kuzuka kwa mzozo mpana zaidi katika eneo la Pembe ya Afrika , huku Sudan ikiwa inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopelekea watu milioni 14 kuyakimbia makazi yao tangu Aprili mwaka 2023.
China yatoa wito wa utulivu
China imesema ina matumaini kuwa hali ya usalama katika eneo la Pembe ya Afrika itaimarika hivi karibuni na kwamba iko tayari kushirikiana na pande zote kuimarisha amani na utulivu wa kanda hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi maalum wa China anayeshughulikia masuala ya Afrika, Liu Xianfa, wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia.
Hii ni baada ya uhusiano kuendelea kuzorota baina ya Ethiopia na Sudan zikituhumiana kuwaunga mkono waasi na hivyo kuyumbisha usalama katika eneo la Pembe ya Afrika.
China imesema itawatuma mwezi huu wajumbe wake katika nchi za Afrika na huko Mashariki ya Kati kwa ziara mbalimbali.
Lengo la ziara hizo ikiwa ni kusaidia michakato ya mazungumzo, kupunguza hali ya mvutano wa kisiasa na kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhu ya migogoro katika maeneo hayo.
