
Na Nyamiti A, Nyamiti
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga, wamemlalamikia mkandarasi wa kampuni ya SIHOTECH ENGINEERING COMPANY LIMITED Vs MPONELA CONSTRUCTION AND COMPANY LIMITED, Anayetekeleza Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria, kwa kushindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 6, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Oktoba 7, 2026. Hata hivyo hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 37.5 tu, na mkandarasi ameongezewa mkataba wa mwaka mmoja hadi Aprili 6, 2028.

Diwani wa Kata ya Kinamapula, Mhe. Samweli Adriano, amesema kutokana na changamoto ya maji katika Jimbo la Ushetu, wananchi kwenye baadhi ya maeneo wamekuwa wakilazimika kuchangia chanzo kimoja cha maji na mifugo kwa pamoja hasa kipindi cha kiangazi, hali inayohahatarisha afya zao.
Akijibu malalamiko hayo, Mwakilishi wa Meneja kutoka Taasisi ya RUWASA, Eng. Mkama Msilanga, amesema mradi huo katika hatua ya kwanza unatekelezwa katika kata 11 na unagharimu kiasi cha Tsh Bil 37.5.
Msilanga ameeleza kuwa hadi sasa matanki 3 yenye ujazo wa lita laki 1, laki 3 na laki 5 yamekamilika katika Kata ya Ulowa, na sasa wanatarajia kuanza zoezi la kulaza mabomba kwenda kwenye vijiji husika.
Madiwani hao wameitaka RUWASA kumsimamia kikamilifu mkandarasi huyo ili mradi ukamilike ndani ya muda wa nyongeza uliotolewa, ili kuondoa adha ya maji kwa wananchi wa Ushetu.

