
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuondoka nchini leo, Novemba 10, 2026, kuelekea jijini Antalya, nchini Uturuki, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).
Akiwa nchini humo, Rais Samia atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Antalya Leaders’ Summit), pamoja na kikao cha ngazi ya juu kinachohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika (High-Level Event on Clean Cooking in Africa).
Aidha, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki.
Mkutano wa COP31 unaendelea nchini Uturuki ukiwakutanisha viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kujadili hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unatarajiwa kutoa fursa ya kuendeleza msimamo wa nchi katika masuala ya mazingira, nishati safi na maendeleo endelevu.

