
Na Nyamiti A. Nyamiti
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefungua huduma ya Viwango Clinic katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, kwa lengo kutoa elimu ya ubora wa bidhaa kwa wafanyabiashara wa viwanda vya kuzalisha vyakula, Maduka ya vyakula na wamiliki wa maduka ya vipodozi.
Akifungua Clinic hiyo Katibu Tawala Wilay ya Kahama GLORY ABSALUM, amewapongeza TBS kwa uamuzi wa kusogeza huduma karibu na wananchi katika maeneo ya biashara na kutoa elimu ya usalama wa chakula na vipodozi kwa ustawi wa watumiaji.
ABSALUM amewataka wafanyabiashara kujitokeza kusajiri biashara zao ili kukidhi vigezo na kuitumia TBS kama sehemu ya kutanua wigo wa biashara.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Baraka Msumi, Amesema Kahama kumekuwa na ongezeko kubwa la viwanda vinavyozalisha bidhaa za chakula, hivyo ni muhimu bidhaa hizo ziwe na ubora unaokubalika kwa matumizi salama ya binadamu.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa na Magharibi, JOSEPH MAKENE, Amesema lengo la kampeni ya Viwango Clinic iliyoanza Novemba 16 hadi 20 ni uhamasishaji wa kusajili bidhaa, uthibitishaji wa bidhaa na usajiri wa leseni za kutumia Nembo ya Ubora ya TBS.

Naye KADO ANDRWEA, Mfanyabiashara wa kusindika mchele, amesema baada ya kusajiri biashara yake na kuanza kutumia nembo ya TBS, amefanikiwa kupata masoko hadi katika mataifa ya Uganda na Burundi.
Kwa upande wake, LATIFA NAZIRI SHABAN, mfanyabiashara wa duka la vipodozi la Forever Young – Skin Care Mtaa wa Masabo Kahama, amesema elimu anayoipata kutoka TBS imemsaidia kutoa huduma bora kwa wateja wake ambao sasa wanafurahi kuwa sehemu ya biashara yake.

