Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amepongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuwa mfano bora wa utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia nchini.
Amesema kuwa STAMICO imeonyesha mwelekeo sahihi kupitia uzalishaji wa mkaa mbadala uitwao Rafiki Briquettes, unaotokana na makaa ya mawe.
Dkt. Mpango amesema hayo, Februari 21, 2025 wakati akifunga mkutano wa mafunzo wa 109 wa watayarishaji wa Vipindi vya Elimu kwa Umma (WASHITIRI) kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) chini ya Uenyekiti wa STAMICO uliofanyika katika Ukumbi wa City Park Garden uliopo Jijini Mbeya.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imejipanga kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira. Amesema kuwa Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 8.68 kwa ajili ya upatikanaji wa nishati hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa wa miti ambao unachangia uharibifu wa mazingira.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni moja ya vipaumbele vya Taifa letu. Tunataka ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi, kama vile gesi asilia, umeme wa jua, na mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes unaotengenezwa na STAMICO,” amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amefafanua kuwa tangu Serikali ilipotoa katazo kwa taasisi zote za umma zinazohudumia watu wasiopungua 100 kwa siku kuacha matumizi ya kuni na mkaa wa miti, tayari taasisi 506 zimekwishaanza kutumia nishati safi ya kupikia. Amezitaka taasisi nyingine zinazobaki kuhakikisha zinaharakisha mchakato wa kuhama ili kulinda afya za watumiaji na kusaidia juhudi za uhifadhi wa mazingira.
“Natoa wito kwa taasisi zote za umma zinazohudumia watu wasiopungua 100 kwa siku, kuhakikisha zinafuata maelekezo haya haraka iwezekanavyo. Serikali iko imara katika kuhakikisha mabadiliko haya yanafanikiwa kwa manufaa ya taifa letu,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika hatua nyingine, Shirika la STAMICO limeingia ubia na Taasisi ya Wanawake na Samia, kwa kuwapatia uwakala wa usambazaji wa Rafiki Briquettes. Taasisi hiyo, ambayo inafanya kazi katika mikoa 20 ya Tanzania Bara na mkoa mmoja wa Zanzibar, imetambuliwa kwa juhudi zake za kuwawezesha wanawake kushiriki katika sekta ya nishati safi.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais, Dkt. Mpango, amekabidhi rasmi vyeti vya uwakala kwa wawakilishi wa wanawake hao kutoka mikoa ya Songwe, Iringa, Njombe, na Ruvuma. Aidha, jumuiya ya wazazi kutoka Mbinga na wafanyabiashara wa Soko la Mwanjelwa pamoja na Mkoa wa Mbeya walipokea vyeti hivyo kwa kutambua mchango wao katika kusambaza Rafiki Briquettes.
Kwa kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika taasisi za elimu, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amekabidhi majiko matatu ya kisasa kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza jijini Mbeya. Majiko hayo, ambayo yana uzito wa kilogramu 50 kila moja kutoka STAMICO yanatarajiwa kupunguza gharama za nishati shuleni hapo na kuboresha mazingira ya upishi kwa wanafunzi.
Juhudi za Serikali na wadau kama STAMICO zinaonyesha dhamira thabiti ya kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi. STAMICO kupitia uzalishaji wa Rafiki Briquettes na uwezeshaji wa wanawake katika usambazaji wa bidhaa hizo, Tanzania imepanga kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa miti kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Mkutano huo umefanyika chini ya Kaulimbiu ya “Tumia Nishati Safi, Tunza Mazingira”