Nahodha wa kikosi cha Simba SC, Mohamed Hussein almaarufu “Tshabalala”, ameandika ujumbe wa kugusa moyo akiwaaga mashabiki na kutoa shukrani kwa uongozi wa klabu hiyo baada ya msimu kukamilika rasmi.
Katika ujumbe wake, Tshabalala amesema:
“Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kutuwezesha kuanza ligi na kumaliza salama. Pili, uongozi chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohammed Dewji na makamu wake Murtaza Mangungu, benchi la ufundi, menejimenti, wanachama na mashabiki wote kwa kuwa bega kwa bega nasi mpaka mwisho wa msimu.”
Akiwageukia mashabiki wa timu hiyo, Tshabalala amesema hana maneno ya kuelezea mapenzi yake kwao:
“Kwa mashabiki wetu, sijui nitumie maneno gani kuelezea shukrani zangu za dhati kwenu kwa mapenzi yenu makubwa kwetu. Hakika tuna deni la kulipa kwenu. Siwezi kulinganisha na kitu chochote kwenye suala la kutupa nguvu na kutupigania ndani na nje ya uwanja. Iwe jua kali au mvua, mlikuwepo. Katika kila nyakati ngumu hamkukata tamaa, hamkutuacha. Mwenyezi Mungu awabariki sana. You are the true heroes.”
Akimalizia, Tshabalala amesema msimu huu ukifungwa ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mpya:
“Mwisho wa msimu mmoja ndio maandalizi ya msimu mwingine. Inshallah, next season tutafanya vizuri zaidi.”
Kauli hiyo imepokewa kwa hisia mbalimbali mitandaoni huku mashabiki wengi wakimpongeza kwa uongozi wake na kujituma uwanjani.