
Ni sauti zilizobeba furaha na shukrani, Sauti za baraka baada ya wananchi wa Kahama kuhakikishiwa kesho yenye mwanga wa elimu bora na mafanikio.
Hii ni ishara ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, utekelezaji wa ilani umejidhihirisha katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Barabara, Masoko, Nishati pamoja na utoaji wa mikopo kwa Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu.
Moja ya mafanikio makubwa ni ujenzi wa shule mpya, zikiwemo Shule ya Sekondari Amali Lowa na Wendele, zilizopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata elimu.
Shija Butemi, mwanafunzi wa Amali Lowa, anakumbuka changamoto walizopitia kabla ya shule hiyo kujengwa:
“Mwanzoni tulisoma Sekondari ya Nyandekwa, Tulikuwa tunapata tabu kubwa, hasa sisi wasichana, Mara nyingi tulitembea kwa miguu, na wakati mwingine tulilazimika kuomba msaada kwa bodaboda ambao walituuliza ‘mnatupa nini?’ Hali hii ilisababisha baadhi ya wenzetu kushawishika vibaya na kuishia kupata mimba, Tunamshukuru Rais Samia kwa kutujengea shule ya karibu, sasa tunafika mapema na masomo yamekuwa rahisi.”
“Awali tulikuwa tukisafiri kutoka kijiji cha Tumaini hadi Sekondari ya Ngogwa, umbali mrefu uliotusababisha uchovu na kushuka ufaulu, Shule hii mpya imetupunguzia changamoto hizo, Naomba wazazi waache kuwazuia watoto wao waende shule; elimu ndiyo urithi wa kweli.”
Shija Bundala, mwanafunzi mwingine wa Amali Lowa, pia anawataka wenzake walioacha shule kwa sababu ya umbali warejee sasa kwa kuwa shule ipo jirani.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule ya Amali Lowa, Mwalimu Ezekia Ngabo, anasema shule hiyo ilianza rasmi Julai 28, 2025 ikiwa na wanafunzi 47 (wavulana 13 na wasichana 34) na walimu 9 pamoja na mlinzi mmoja.
“Shule hii ina mikondo miwili: wa jumla na wa amali (elimu ya vitendo), Kupitia mkondo wa amali, hasa somo la kilimo, tunawajengea wanafunzi stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.”
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, anabainisha kuwa mafanikio haya ni matunda ya ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Halmashauri:
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwekea mazingira bora ya ukusanyaji mapato na kutupatia fedha za maendeleo. Tulipokea zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za Wendele na Amali Lowa, zikiwa na madarasa, jengo la utawala, maabara na vyoo, Ujenzi umekamilika na wanafunzi wameanza kusoma, Huu ni ushahidi wa dhamira ya serikali kuwekeza kwenye elimu bora.”
Masudi ameongeza kuwa miradi mingine ya maendeleo katika sekta za afya, barabara na maji imeendelea kuipamba Manispaa ya Kahama, na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Wananchi wa Kahama sasa wananufaika moja kwa moja na miradi ya elimu, afya, na miundombinu, matunda ya Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Changamoto bado zipo, kama vile mahitaji ya walimu na vifaa vya kisasa vya kujifunzia, lakini matumaini yamejengeka, Ndoto za watoto wa vijijini kupata elimu bora sasa zinageuka kuwa uhalisia.
Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu ili miradi ya maendeleo iendelee.