
Na Nyamiti A, Nyamiti.
Kufuatia changamoto ya ukosefu wa Ofisi ya Utawala katika Kijiji cha Magobeko, Kata ya Kinaga, Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, wananchi wamehamasika na kuanza ujenzi wa vyumba 3 kwa ajili ya kusogeza huduma za kijamii karibu.
Wakizungumza kupitia mkutano wa kijiji, wakazi hao wamesema uamuzi huo umekuja kufuatia changamoto kubwa ya kukosa huduma kwa wakati na kulazimika kutumia sehemu ya mapato ya kijiji Kulipia jengo wanalotumia kupatia huduma kwa Mda.
Diwani wa Kata ya Kinaga, Mhe. Gerald Joseph, ameunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia mifuko 12 ya saruji yenye thamani ya Tsh. 312,000/ na kusisitiza wananchi kuendelea kuchangia ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mtendaji wa Kijiji cha Magobeko, Wilson Mpuya, ametaja hatua iliyofikiwa ya mradi huo kutokana na michango iliyotolewa na wananchi hadi sasa na kueleza kuwa kazi inaendelea vizuri licha ya changamoto ya Baadhi ya wakazi kusuasua kwenye Uchangiaji.
Wananchi wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia kukamilisha jengo hilo muhimu kwa maendeleo ya kijiji.
