Ndege mbili za Shirika la Ndege la Precision Air zimeshindwa kufanya safari zake kama kawaida baada ya ndege moja kupata hitilafu na nyingine kulazimika kutua kwa dharura.
Taarifa rasmi iliyotolewa na shirika hilo asubuhi ya leo Februari 03, 2023 imeeleza kuwa, moja ya ndege zake ilipata hitilafu ya kiufundi hivyo kusababisha kuchelewa na kuahirishwa kwa safari.
Shirika hilo limesema kuwa, ndege nyingine ya Precision Air ililazimika kutua kwa dharura baada ya kugonga kiumbe aina ya ndege kama kunguru au njiwa wakati ikiruka kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Taarifa hiyo inamalizia kwa msisitizo wa kuomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza huku shirika likifanya jitihada za kurejesha safari hizo kama kawaida.
Taarifa hiyo inasomeka; “Tunapenda kuwataarifu wateja wetu pamoja na umma kwa jumla kwamba moja ya ndege zetu imepata hitilafu ya kiufundi hivyo kusababisha kuchelewa na kuahirishwa kwa baadhi ya safari zettu.
“Katika tukio lingine, ndege yetu yenye usajili namba 5H-PWD ililazimika kutua kwa dharura baada ya kugongana na ndege (kama njiwa au kunguru) wakati ikiruka kuelekea Dodoma ikitokea Dar es Salaam.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza, tunafanya jitihada za dhati kurejesha safari zetu katika hali ya kawaida.”
Matukio hayo yanajitokeza ikiwa ni miezi kadhaa tangu ilipotokea ajali mbaya ya ndege ya Presicion Air mwezi Novemba mwaka jana ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19.