YANGA hawatanii kimataifa ndivyo unavyoweza kusema, hii ni baada ya uongozi wa timu hiyo kuweka wazi kuwa unatarajia kutumia siku tano sawa na saa 120 ndani ya nchi ya Tunisia, kwa ajili ya maandalizi yao kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir.
Yanga ambao wanasalia kuwa wawakilishi pekee wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho mpaka sasa, wanatarajia kuanzia ugenini dhidi ya US Monastir katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi, ambao unatarajiwa kupigwa Februari 12, mwaka huu.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara katika mashindano hayo wamepangwa kwenye kundi D, pamoja na timu za TP Mazembe ya DR Congo, US Monastir ya Tunisia na Real Bamako ya Mali, huku wakiweka wazi kikosi chao kinatarajiwa kusafiri kati ya Jumatatu au Jumanne wiki ijayo.
Akizungumzia Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alisema: “Mara baada ya mchezo wetu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo tunatarajia rasmi kuanza ratiba yetu ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo tunatarajia kucheza mchezo wetu wa kwanza Februari 12, mwaka huu dhidi ya US Monastir nchini Tunisia.
“Katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mchezo huu, uongozi umejipanga kuipeleka timu Tunisia siku tano kabla ya mchezo kwa ajili ya kuweka taratibu zote sawa ikiwemo kuzoea mazingira ya baridi kali lililoko nchini Tunisia kwa sasa.”