KIUNGO mshambuliaji wa Yanga Mghana, Bernard Morrison ameondolewa katika mipango ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi kutokana na maumivu ya nyonga.
Mghana huyo alikuwepo katika kambi ya timu hiyo, iliyoweka huko Avic Town, Kigamboni jijini Dar kabla ya kuondolewa na Nabi kutokana na majeraha hayo.
Nyota huyo amekuwa hana mfululizo mzuri wa kucheza michezo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA kutokana na ruhusa za kila wakati na majeraha.
Akizungumza Jumatatu, Nabi alisema kuwa kiungo huyo amemuondoa kambini kutokana na kutokuwa katika mipango ya kucheza ligi na michuano ya kimataifa.
Nabi alisema kuwa ripoti iliyotolewa na madaktari wa timu hiyo, kiungo huyo atakaa nje ya uwanja kwa muda miezi miwili.
Aliongeza kuwa kukosekana kwa kiungo hakuifanyi timu hiyo, iyumbe kutokana na kuwepo viungo wengine wa aina yake wenye kiwango bora kama chake.
“Morrison hajaonekana katika mchezo huu wa ligi dhidi ya Namungo kutokana na maumivu ya nyonga aliyoyapata mazoezini.
“Hivi sasa yupo katika matibabu yatakayomrejesha haraka uwanjani kuipambania timu yake, na hivyo nimemuondoa katika kikosi changu.
“Ninaamini wachezaji waliokuwepo kuwepo katika kiwango bora, hivyo kukosekana kwake kunawapa nafasi wachezaji wengine waliokuwepo kikosini kwangu,” alisema Nabi.