Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amewatoa hofu wananchi kutokana na taarifa ya kuwepo kwa ajali ya ndege akisema yalikuwa ni majaribio kwa ajili ya kupima utayari wa kuokoa katika matukio kama hayo yanapotokea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13 wilayani hapa, DC Mhita amesema jaribio hilo limeratibiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kwamba hufanyika kila baada ya miaka miwili na leo ilikuwa ni zamu yakiwanja cha ndege cha Kahama.
Mbali na utayari katika viwanja vya ndege, wananchi wameshauri kuwa utaratibu wa kufanya mazoezi ya utayari uwekwe wazi ili kuepusha taharuki na madhara mengine yanayoweza kutokea.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi kuhusu majaribio hayo wamesema taarifa za ajali zilizosambaa kwenye mitandao ya jamii na baadaye kukanushwa zitawafanya wananchi kupuuza matukio hayo endapo yatakuja kutokea kwa uhalisia.
“Kama kwenye taasisi wanafanya mazoezi kama hayo kwa nia ya kujiweka sawa katika janga lolote ambalo linatokea katika nchi yanafaa, ila lazima kuwe na tahadhari kwa sababu wakiwa wana wanafanya kwa wananchi, wanaweza kujua ni janga ambalo kweli limetokea,” amesema Peter Kasanzu ambaye ni mkazi wa jijini Mwanza.
Ameongeza; “Ila kumbe sio kweli, watu wengine wakapata taharuki ikasababisha majanga mbalimbali kama mtu alikuwa na ndugu yake anasafiri kweli kwenye njia hiyo akapata presha.”
Naye Masoud Amrani amesema kutokana na taarifa za majanga kuripotiwa kisha mamlaka kukanusha mwishowe watu wataanza kuzipuuza hata kama zitatokea kweli hiyo kuleta madhara mengine.
“Mtu unajua mke wako yupo ofisi fulani alafu unasikia imewaka moto na watu 10 wamefariki hivi anapokeaje hivyo vitu? Anapata presha alafu baadaye zinakuja taarifa za majaribio ya utayari? Huu utaratibu ubadilishwe,” amesema Masoud.
Naye Hazina Mzirayi amesema “Kwa mimi navyoona majaribio ya utayari yanayofanywa ghafla yanazua taharuki sio tu kwa jamii ambayo inazunguka hayo maeneo au wana mahusiano na hao watu pia kwa watu wenyewe kwakuwa yanaweza kuzua tatizo badala ya kumaliza tatizo,” amesema.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema hakuna watu waliokufa kwa ajali ya ndege Kahama isipokuwa yalikuwa ni mazoezi kwa vitendo ya kujiweka tayari kukabiliana na majanga ya moto.
Amewaondoa hofu wananchi akisema yalikuwa ni majaribio ya utayari kwa matukio ya ajali.