Siku moja baada ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kudai kuwa ndege sita za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) hazitumiki kwa sababu ya hitilafu, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Ladislaus Matindi amefafanua kuwa ni ndege tatu zenye matatizo.
Amefafanua kuwa kati ya ndege hizo, mbili zina kasoro za kiufundi kwenye injini na moja ina matatizo ya kisheria.
Jana katika uzinduzi wa mikutano ya hadhara iliyofanyika katika uwanja wa Mbagala Zakheim, Zitto alisema anazo taarifa kuwa ndege sita kati ya 11 hazifanyi kazi kutokana na ubovu uliosababishwa na mtengenezaji.
Zitto alitaka ufanyike uchunguzi wa ununuzi wa ndege hizo na masuala mbalimbali yaliyofanyika katika kipindi cha utawala wa John Magufuli, Rais aliyezuia mikutano ya hadhara ambayo ingeweza kuibua madudu ya Serikali.
Akizungumzia hali ya utoaji wa huduma wa ndege leo Jumatatu Februari 20, 2023 jijini Dar es Salaam, Matindi ambaye hakumtaja mtu, amesema ndege mbili ndizo zenye matatizo ya kiufundi yaliyotokana na mtengenezaji na moja ina changamoto ya masuala ya kisheria huku nane zikifanya safari maeneo tofauti ikiwemo India na China.
“Tuna ndege nane zinazofanya kazi bila matatizo, zisizofanya kazi kwa matatizo ya kiufundi ni mbili, tatizo ni la watengenezaji… mnaweza kufuatilia kuhakikisha maneno.
“Kama mnataka kuhakikisha nendeni uwanja wa ndege, tena mkifika angalieni kwenye mkia ambako kuna namba imeanzia 5h kisha angalia namba.
“Inawezekana kukawa na matengenezo ya lazima, hayo ni kama gari lako likifika kilomita. Hatuna kificho hizi ni ndege za Watanzania ni haki yao kujua ziko wapi na zinafanya kazi gani,” alisema.
Desemba 2022, Serikali iliwatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa za kushikiliwa kwa ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nchini Uholanzi, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi inayoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Katika mkutano wake wa juzi, Zitto alidai kuwa ATCL imeandika barua serikalini kukodisha ndege ili ziweze kuziba pengo la safari zilizokuwa zikifanywa na ndege sita zilizosimama kwa ajili ya ubovu.
“Huu ni ufisadi yaani ndege sita zote ni mbovu, tunataka uchunguzi maana hela zilizotumika ni za Watanzania. Haya ndiyo madhara ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara,” alisema.