Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini huku akisema ana deni la kufanya kazi kuimarisha imani hiyo kwake.
Chalamila ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Kagera, amehamishiwa Dar es Salaam katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa ambayo Rais Samia aliyafanya jana Mei 15, 2023 kwa kuwabadilisha vituo vya kazi wakuu wa mikoa wanne.
Mbali na kuongoza mkoa wa Dar es Salaam na Kagera, Chalamila aliwahi kuwa mkuu wa Mbeya na Mwanza.
Akizungumzia uteuzi wake, Chalamila amemshukuru Rais Samia na kuahidi kufanya kazi kwa bidi ili kulinda imani ambayo ameiweka kwake.
“Awali ya yote namshukuru Mungu kwa wema wake kwangu na familia. Namshukuru sana Rais kwa imani yake kwangu…Nina deni la kufanya kazi na kuimarisha imani ya Rais kwangu,” amesema Chalamila.
Chalamila amepokea kijiti hicho kutoka kwa Amos Makalla ambaye amehamishiwa mkoa wa Mwanza, katika kipindi ambacho mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo ukiendelea wakilalamikia kodi mbalimbali.
Katika utendaji wake, atakuwa amepata uzoefu wa kuongoza majiji makubwa kama vile Mbeya na Mwanza na sasa anakabiliwa na kibarua cha kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara pamoja na hali ya usafi wa Jiji la Dar es Salaam.