Zikiwa zimepita siku 496 tangu Job Ndugai ajiuzulu uspika wa Bunge, amesema Waziri Mkuu mstaafu, John Malechela ndiye alimshawishi kuchukua uamuzi huo.
Alitoboa siri hiyo katika mazishi ya William Malecela, maarufu ‘Le Mutuz’, mtoto wa Malecela, yaliyofanyika Mvumi, wilayani Chamwino mkoani hapa na kuhudhuriwa na viongozi wa kisiasa, Serikali na Bunge.
Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa, alichukua uamuzi wa kujiuzulu Januari 6, mwaka jana kwa kumwandikia barua katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kujiuzulu kwake kuwa kiongozi wa muhimili huo wa Bunge.
Uamuzi huo aliuchukua baada ya kauli aliyokuwa ameitoa Desemba 26 mwaka juzi katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma kuibua mjadala mkali ndani ya CCM na serikalini.
Katika mkutano huo, Ndugai ambaye ni mwanasiasa mkongwe, alihoji wanaofurahia nchi kukopa na kwamba deni limefika Sh70 trilioni ambalo ni kubwa na Serikali ikiendelea kukopa, “kuna siku nchi itapigwa mnada hii.”
“Juzi mama ameenda kukopa Sh1.3 trilioni. Hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru, kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapahapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alihoji Ndugai Desemba 2021.
Kauli hiyo ilikosolewa na makada mbalimbali wa CCM pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyesema lazima Serikali ikope ili kumaliza miradi ya maendeleo.
Rais Samia alisema kwa kuwa fedha zinazokopwa zinakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo, Serikali itaendelea kukopa.
Katikati ya mjadala mkali kutoka kwa makada wa CCM, wakiwamo viongozi wa mikoa na wabunge, Ndugai akatangaza kujiuzulu kupitia taarifa yake kwa umma. CCM ilimteua naibu spika, Dk Tulia Ackson kumrithi Ndugai na Bunge likamchagua kwa kishindo.
Akizungumza kwa kifupi msibani hapo jana, Ndugai alisema, “kwa nini nimeuchukulia msiba huu kwa uzito, mwaka jana Januari wiki ya kwanza, mzee Malecela alikuja nyumbani kwangu Kongwa kwenye saa mbili au tatu usiku. Nikamkaribisha lakini nikashangaa mbona mzee amekuja usiku?”
Alisema alimkaribisha (mzee Malecela) kwa sababu ilikuwa mwanzo wa mwaka na alikuwa likizo, Malecela aliomba chai ya rangi na kumweleza amekuja kwake kama kaka yake.
Ndugai alisema alimweleza kuwa ni lazima kesho ajiuzulu kwenye nafasi ya uspika ili kulinda heshima yake.
“Aliniambia nadhani ni vizuri kesho ukajiuzulu uspika na jambo hilo usikose kufanya, sikumuuliza swali na sijamuuliza mpaka leo, kesho yake nilijiuzulu uspika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Ndugai
Alisema hali hiyo inaonesha kwa jinsi ambavyo waziri mkuu huyo mstaafu ana uzito katika maisha yake.
Wakati Ndugai akizungumza, mzee Malecela na mkewe, Anne Kilango walikuwa wamekaa mita chache wakimsikiliza na alipomaliza kuzungumza alikwenda walipokuwa wamekaa kuwapa mkono.
Le Mutuz alifariki dunia Mei 14 mwaka huu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua ghafla. Ameacha mke na watoto wawili.
Akizungumza katika mazishi hayo, Spika wa Bunge, Tulia Ackson alisema amemfahamu marehemu Le Mutuz kama mtu mwema, huku akiwataka wanaoendelea kubaki duniani kuendelea kutenda matendo mema.
“Alikuwa na usemi wake wa case closed, hili la case closed alikuwa na namna alivyokuwa akilitumia, jambo likianzia mahali na amelielewa alikuwa analitumia na mnaongea kwenye simu anasema case closed, leo tunamuaga ndio case closed yake,” alisema Spika Tulia.
Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Alhaj Abdallah Bulembo alisema amemfahamu kwa muda mrefu marehemu Le Mutuz na alimpokea Jumuiya ya Wazazi akitokea Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (UVCCM).