Jeshi la Polisi mkoani Tabora linaendelea na uchunguzi kufuatia utata wa vifo vya watoto mapacha ambao walizaliwa njiti katika kituo cha afya Kaliua kilichopo mkoani humo ambapo mtoto mmoja alikutwa ameondolewa ngozi ya paji la uso na kuharibiwa jicho moja la upande wa kulia.
Taarifa hiyo imetolewa hii Mei 18, 2023, na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora ACP Costantine Mbogambi.
Amesema watoto hao baada ya kufariki dunia wakiwa katika kituo cha afya wanafamilia walikabidhiwa miili ya watoto hao ambapo kabla ya kuwazika mmoja alionekana akiwa amechunwa ngozi ya paji la uso pamoja na kuharibiwa jicho moja la upande wa kulia .
Mpaka sasa miili ya watoto hao bado imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo baada ya wanafamilia kukataa kufanya maziko mpaka uchunguzi wa mzingira ya kifo cha watoto hao utakapokamilika.