Wastani wa wanawake 2,700 huugua ugonjwa wa Fistula nchini Tanzania kila mwaka huku wagonjwa 1,000 wakikosa matibabu ya ugonjwa huo.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonyesha nchini Tanzania kuna wanawake kati ya 10,000 na 20,000 wanaougua Fistula.
Hata hivyo, ukata na huduma duni ikiwemo ukosefu wa vifaa kwa ajili ya upimaji na upasuaji wa fistula unatajwa kuchangia wanawake hao kukosa huduma ya matibabu ya ugonjwa huo.
Kufuatia changamoto hiyo, Shirika la Americares Tanzania limetoa msaada wa vifaa tiba vya upasuaji wa Fistula ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa (Bugando) vyenye thamani ya Sh234 milioni.
Akizungumza jana baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo, Dk Nguke Mwakatundu alisema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha kila mwanamke anayeugua fistula Kanda ya Ziwa anapata matibabu kwa wakati.
“Vifaa hivi vitaboresha huduma za upasuaji na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na upasuaji wa Fistula. Lengo ni kutokomeza ugonjwa wa Fistula nchini ifikapo 2030,” alisema Dk Mwakatundu
Mbali na kutoa msaada wa vifaa hivyo, Dk Mwakatundu alisema shirika hilo limewajengea uwezo watoa huduma katika hospitali ya rufaa ya Bugando ili kuwawezesha kufanya utambuzi wa wanawake wenye Fustula kupitia ‘Huduma Mkopa’ katika mikoa ya kanda hiyo.
“Tutahakikisha hakuna mwanamke anayefedheheka kutokana na ugonjwa huu. Tutahakikisha wanapatiwa mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, malazi na mavazi hivyo wanawake wanaohisi kusumbuliwa na Fustula wajitokeze Bugando kupatiwa matibabu hayo,” alisema
Mkurugenzi Mkuu wa Bugando, Dk Fabian Massaga alisema kwa mwaka 2022, Bugando ilihudumia wanawake 373 wenye tatizo la Fistula ambapo 207 kati yao walifanyiwa upasuaji huku 166 wakipatiwa tiba ya viungo.
Alisema asilimia kubwa ya wagonjwa hao wanatokea mkoani Geita na Shinyanga kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa huku mwamko wa kupima ugonjwa huo ukitajwa kuchangia idadi hiyo.
“Pamoja na juhudi tunazozifanya kuhakikisha kila mgonjwa wa Fistula anapatiwa matibabu lakini tunahitaji wadau watushike mkono ili kutoa huduma inayohitajika. Tunasashukuru Americares Tanzania kwa kutushika mkono,” alisema Dk Massaga
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla aliishukuru Americares Tanzania kwa msaada huo huku akiitaka Bugando kuvilinda ili vilete tija na ufanisi wa matibabu ya Fistula kwa muda mrefu.