Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa umeruhusu kwa masharti, matumizi ya nyama na mazao ya nguruwe, baada ya kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe iliyokuwa imeikumba wilaya hiyo.
Akizungumza leo Juni 2, 2023 Afisa Kilimo Mifugo na Uvuvi Festo Mkomba amesema mnyama huyo ameruhusiwa kuchinjwa pamoja na kutumika kwa mazao yake kwa sharti la kutotoa mazao hayo nje ya kijiji ambacho mnyama huyo amechinjwa.
Amesema nguruwe yeyote atapaswa kufanyiwa ukaguzi masaa yasiyo pungua 48 kabla ya kuchinjwa kwake.
“Ukaguzi wa awali ufanyike masaa 48 kabla ya kuchinjwa na ufanywe na mtaalamu aliye idhinishwa katika eneo husika, na nguruwe atakaye onesha dalili za aina yeyote ya ugonjwa, taarifa zitolewe kwa wataalamu wa eneo husika.” Amesema Mkomba.
Ameongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya nguruwe 417 wamekufa kwa ugonjwa huo na wamefanya jitihada za kutosha kuhakikisha ugonjwa huo hauenei.
“Tumekuwa tukioa elimu na kupita kukagua nguruwe katika maeneo mabalimbali ya wilaya hii na tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa huu japo haikuwa rahisi kwakuwa kuna baadhi ya watu wasio waaminifu walikuwa wakichinja kwa siri na kuuza nyama hiyo huku wakiwa wameipa jina la Mbolea ya Ruzuku ili wasigundulike kwa urahisi,” amesema Mkomba.