Kapteni Neema Swai amekuwa kivutio kwa watu wengi baada ya kurusha ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F kutoka Seattle, Marekani hadi Dar es Salaam, umbali wa maili 9,432.
Hata hivyo, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 33, ana mengi yasiyojulikana yanayomfanya kuwa wa kipekee si tu katika tasnia ya urubani, bali pia katika maisha ya kawaida ya kila siku.
Juni 3, Rais Samia Suluhu Hassan aliipokea ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kushushwa na Kapteni Neema, aliyekuwa rubani kiongozi katika safari hiyo.
Baada ya kushusha ndege hiyo katika ardhi ya Tanzania majira ya saa 8:55 mchana, Kapteni Neema na marubani wasaidizi kutoka Kampuni ya Boeing ya Marekani, walishuka na kwenda jukwaa kuu kupongezwa na Rais Samia.
Uwezo wa mwanamke huyo umedhihirika kwa kuwa anafanya kazi katika tasnia iliyotawaliwa na wanaume kwa muda mrefu, hivyo fursa hiyo ya kwenda kuileta ndege imeonyesha uwezo wake binafsi na wa wanawake.
Katika mahojiano yake na Mwananchi, Kapteni Neema anasimulia maisha yake ya kitaaluma na binafsi akisema hakusoma darasa la saba kutokana na shughuli za wazazi wake.
Kapteni Neema anasema alipata elimu yake Kenya na Uganda kwa nyakati tofauti kabla ya kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya masomo ya urubani na kufanikiwa kupata kazi ndani ya muda mfupi.
Anasema alisoma Shule ya singi Juja iliyopo Nairobi, Kenya na alifika hadi darasa la sita, wazazi wake walihamia Uganda, aliwafuata na kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Kaboja.
Katika mfumo wa Kenya, elimu ya msingi inakwenda hadi darasa la nane, hata hivyo hakusoma darasa la saba na la nane, badala yake alijiunga moja kwa moja na sekondari ambako nako alifanya vizuri.
“Sikuwahi kusoma la saba, nilijikuta nimeenda Uganda, nikapewa mtihani wa form one (kidato cha kwanza) nikafaulu, nikaingia form one,” anasema Kapteni Neema wakati akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu.
Anasema baada ya kumaliza kidato cha sita Uganda, alikwenda Afrika Kusini kujiunga na Chuo cha Urubani cha Blue Chip Flight School kwa miezi tisa na kuhitimu mafunzo yake na kuwa rubani.
Kapteni Neema anasema mwaka 2009 baada ya kumaliza masomo yake, aliajiriwa kama rubani akiwa na umri wa miaka 19, alianza kuendesha ndege na ya kwanza kurusha akiwa peke yake ni ATR72-500. “Mimi nilipata bahati, baada ya kumaliza chuo nilipata kazi. Nasema ni bahati kwa sababu wakati huo kampuni zilikuwa zimefunguka kuajiri watu na kuna wengine walikuwa wameacha kazi kwenye hiyo kampuni (hakuitaja), kwa hiyo nikapata kazi,” anasema mwanamke huyo.
Rubani kiongozi mwanamke
Katika Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), kuna marubani 11, Kapteni Neema ndiye rubani kiongozi mwanamke pekee nchini na hajawahi kuwepo mwingine.
Anasema kwenye ndege kuna rubani msaidizi na rubani kiongozi ambao wanatofautiana uzoefu katika kazi na kikubwa kinachoangaliwa ni idadi ya saa ambazo rubani amerusha ndege. “Rubani kiongozi ana uzoefu zaidi ya rubani msaidizi na ana leseni inayoitwa ATPL. Tofauti na hayo, yeye anaweza kufanya kazi yangu na mimi natakiwa kufanya kazi yake,” anasema Kapteni Neema.
Anasema kwa uzoefu wake wa miaka 14 sasa, amerusha ndege kwa zaidi ya saa 8,700, jambo linalompa uzoefu na kuwafanya viongozi wake wamwamini na kumpa majukumu kulingana na uzoefu wake.
Kapteni Neema pia ni mwanamke wa kwanza kurusha ndege ya mizigo ya Boeing 767-300F barani Afrika na kwamba ndege hiyo ni ya kwanza Afrika.
“Ndege za mizigo za Boeing 767 zipo katika nchi nyingine pia, lakini zenyewe zimebadilishwa, zilikuwa za abiria lakini sasa zimegeuzwa kuwa za mizigo. Hii ya kwetu yenyewe imetengenezwa moja kwa moja kama ndege ya mizigo, iko peke yake ya aina hiyo,” anasema.
Mchango wa wazazi
Wazazi wa Kapteni Neema wana mchango mkubwa katika taaluma yake ya urubani, anasema mazingira waliyomjengea, hamasa na elimu ndiyo vimemfanya kufikia mafanikio aliyoyapata hadi sasa.
Anasema alipata hamasa ya kuwa rubani wakati mama yake, Sikudhani Swai alipokuwa akiuza dawa katika duka la dawa lililokuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), jambo lililomuweka karibu na marubani.
Kapteni Neema anasema mara nyingi alikuwa akienda kwa mama yake, alikuwa akiwaona marubani wakitembea uwanjani hapo na kumwambia mama yake, “natamani kuwa rubani”, ndoto ambayo ameifikia.
“Wazazi wangu wana nafasi kubwa kwenye kazi yangu na pia kwenye maisha yangu, nadhani wataendelea kuwa na hii nafasi hadi mwisho wa maisha yangu. Bila wao nisingeweza kufika hapa, wamechangia kwa kunisomesha, kunihamasisha kwenye hii kazi, kunionyesha jinsi ya kujituma,” anasema Kapteni Neema.
Anasema katika miaka 14 ya kufanya kazi ya urubani amefanikisha mengi, ikiwamo kufikia ngazi ya Kapteni, ambayo ndiyo ngazi ya juu katika fani ya urubani, atakachofanya kwa sasa ni kubadilisha ndege tu.
Kapteni Neema anasema ndege ya Boeing 767-300F ndiyo kubwa kati ya zile alizowahi kuendesha na anajivunia kuwa sehemu ya historia kama ambavyo Rais Samia ameandika historia ya kununua ndege ya pekee barani Afrika.
Ameolewa na rubani
Mbali na kuwa rubani, Kapteni Neema pia ni mama wa mtoto mmoja anayeitwa Nana na ameolewa na rubani wa ATCL, Kapteni Khamis Ahmed, anayemtaja kama mmoja kati ya watu anaowahusudu katika fani hiyo. Anasema anatamani siku moja mwanaye afuate nyayo zake na kuwa kapteni, kazi anayoweza kumshauri binti yeyote aifanye kwa sababu urubani siyo kazi ya wanaume, bali hata wanawake wanaweza kuifanya.
“Natamani mtoto wangu awe kama mimi na zaidi ya mimi, niweze kukaa siku moja nimwone mtoto wangu anafika mbali, anakuwa kapteni, anaendesha ndege kubwa kuliko hii (Boeing 767),” anasema.
Anasema anajitahidi kugawa muda wake katika kutekeleza majukumu yake kama kapteni na mama wa familia na anaepusha kuchanganya majukumu hayo kwa sababu ni tofauti na anaiheshimu familia yake.
“Nikiwa kazini naitwa Kapteni, nikiwa nyumbani naitwa mama Nana, hivi ni vyeo viwili ambavyo haviingiliani kabisa. Kwa hiyo, siwezi kuwa kazini nikawa mama Nana na siwezi kuwa nyumbani nikawa Kapteni, haviingiliani. Na ukishaijua hiyo balance basi maisha yanakuwa rahisi,” anasema.
Mwanamke huyo anasema kitu kikubwa anachokipenda katika maisha yake ni kukaa na mwanaye, kucheza naye, kuogelea naye, kumwonyesha vitu vinavyoweza kumfurahisha kama vile wanyama.
“Mtoto wangu anapenda sana kwenda airport (uwanja wa ndege), kila siku ataimba mom take me to the airport (mama nipeleke uwanja wa ndege). Nafurahi kwa sababu naona kama anaingia huku huku ninakotaka aende.”
Changamoto
“Hii industry (tasnia) imetawaliwa na wanaume kwa muda mrefu, kwa hiyo ukija kama mwanamke inabidi ufanye ziada ili wakuamini katika kazi,” anaeleza.
Changamoto nyingine anasema mwanamke akipata ujauzito, anapewa muda fulani wa kufanya kazi kabla hajatolewa katika urushaji wa ndege, unakaa nyumbani hadi utakapojifungua, hivyo katika kipindi hicho anapunguza uzoefu wake.