Mahakama Wilayani Lushoto mkoani Tanga imewahukumu watu watatu kwenda jela miaka 40 kila mmoja kwa makosa ya kukutwa na kijihusisha na nyara za serikali ambazo ni meno matano ya Tembo kinyume na sheria.
Watuhumiwa hao ambao ni Bw. Hassan Kashamba, Elihudi Andrew na Godson Kitau, ambapo wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkuu wa mahakama hiyo Mhe. Rose Andrew Ngoka amewahukumu kwenda jela miaka 40 kila mmoja kwa makosa yote mawili huku kila kosa likichukua miaka 20.
Watuhumiwa hao licha ya kukutwa na meno matano ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 104, pia walikamatwa na pikipiki 2 zenye usajili namba MC 152 CCQ na MC BWQ zilizokuwa zikitumika katika kutenda uhalifu huo.
Waendesha mashtaka kwa upande wa serikali ambao ni Wakili Mwandamizi Bw. Peter Kusekwa akisaidiana na waendesha Mashtaka wa TANAPA Bw. Samwel Magoko na Flavian Kalinga waliieleza Mahakama hiyo kuwa watuhumiwa wote watatu walikamatwa Juni 20, 2022 katika eneo la Hekcho lililopo kijiji cha Manolo wilayani Lushoto.
Kufuatia hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa TANAPA, Flavian Kalinga aliiomba Mahakama kuzitaifisha pikipiki hizo mbili ili liwe ni fundisho kwa watu wengine wanaojiusisha na makosa ya aina hiyo.