Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji katika Kongamano la Kisayansi la Afya ya Magonjwa ya Ini Afrika (COLDA) litakalofanyika Septemba 7 hadi 9, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Jumapili Juni 25, 2023 Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Muhimbili, Dk John Rwegasha amesema kongamano hilo ni la sita barani Afrika na litajumuisha makundi mbalimbali ya wataalamu wa afya.
Dk Rwegasha amesema kongamano hilo linalenga kuzuia maambukizi na usambaaji wa magonjwa ya ini.
“Kongamano lina lengo la kuwawezesha watoa huduma za afya katika nyanja hii ya tiba kutambua magonjwa ya aina mbalimbali yanayoathiri mfumo mzima wa mtiririko wa nyongo,”amesema Rwegasha.
Pia amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wanazuoni na watoa huduma wote kukutana na kushirikiana na wenzao kutoka Mataifa mbalimbali nje ya Bara la Afrika kwa kujadili, kuendeleza na kuboresha tiba ya magonjwa yanayoathiri ini la binadamu ikiwemo virusi vya homa ya ini hususani nchi za Afrika.
Kwa upande wa takwimu amesema kati ya watu 100 ni wanne hadi nane wanaishi na maambukizi ya virusi ya homa ya ini na namba hii inaweza kuongezeka mara mbili zaidi katika makundi hatarishi katika jamii wakiwemo watumia dawa za kulevya wanaojichoma sindano.
“Takwimu kutoka katika hospitali ya Muhimbili saratani ya ini ni ya pili kwa ukubwa na zaidi ya asilimia 60 ya saratani zote pia ilishika nafasi ya saba kwa ukubwa kati ya saratani zote kubwa zinazojulikana na ya tatu kwa ukubwa zinazosababisha vifo kati ya wagonjwa wengi wenye saratani,” amesema Rwegasha.