Jeshi la Polisi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) imemkamata Swamweli Samson mkazi wa Mtaa wa Kihulya Nyakato kata ya Nyasubi kwa tuhuma za kuiba maji na kumwagilia Bustani.
Akiongea na Kahama Fm Afisa Uhusiano wa KUWASA Kahama John Mkama amesema wamepata taarifa za uhujumu huo kwa muda mrefu kutoka kwa wasamaria wema na kwamba walikuwa wanafuatilia ili kubaini ukweli.
Mkama ameongeza kuwa Samson alikuwa anaiba maji hayo majira ya saa kumi alfajiri kwa kumwagilia Bustani, kusafisha banda la Nguruwe na kujaza kisima kilichopo ndani ya nyumba yake.
Mkama Ameongeza kuwa kitendo cha kuchepusha maji ni kosa Kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Maji Namba 5 ya mwaka 2019.
Kwa upande wake Mtendaji wa kata ya Nyasubi Innocent Kapere na mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato Hussein Mwita ambao wamesikitishwa na tukio lililotokea katika Mtaa wao na kutoa wito kwa wananchi wa Mtaa wa Nyakato kuacha tabia ya kuhujumu mali za umma kwani kwa kufanya hivyo ni kuitia hasara serikali na kuikosesha mapato.
Nao baadhi ya majirani walioshuhuduia tukio hilo Mzee John Kihulya Jumanne Mbutuli na Elias Sitta wamesema kuwa wanafahamu jirani yao kuwa ana Bustani ya mbogamboga na wao ni wateja wao licha ya kwamba hawakujua anapata wapi maji ya kumwagilia Bustani hiyo.
Sambamba na hayo wamelaani kitendo hicho cha jirani yao kujiunganishia maji kinyemela na kuwataka watu wengine wenye tabia hiyo kuacha vitendo hivyo.
Kwa upande wake mtuhumiwa wa wizi wa maji Samweli Samson amekiri kuiba maji na kwamba aliamua kufanya hivyo baada ya kuwa na uhaba wa maji kwenye kisima chake.
Samson ameongeza kuwa ameanza kufanya kitendo hicho kwa miezi miwili iliyopita na siyo kweli kama ameanza mwaka Jana na kwamba anaiomba mamlaka imsamehe kwakuwa ni mara yake ya kwanza kufanya kitendo hicho.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama imechukua hatua ya kusitisha huduma ya maji kwa mtuhumiwa huyo na Mtuhumiwa amefikishwa Kituo cha Polisi na Upelelezi utakapokamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.