Wabunge watatu wa upinzani wamepiga kura ya ndiyo kuikubali Bajeti ya Serikali.
Wabunge hao waliopiga kura ya ndiyo ni Nusrati Hanje (Viti Maalumu), Salome Makamba (Viti Maalumu) wote kutoka kundi la wabunge 19 wenye mgogoro na Chadema pamoja na Mbunge wa Mtambile (ACT-Wazalendo), Seif Salim Seif ambaye naye amesema ndiyo.
Tukio hilo limetokea leo Jumatatu Juni 26, 2023 wakati Bunge lilipokuwa likipiga kura ya kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24.
Kanuni za Bunge zinataja kuwa, kura za uamuzi wakati wa upitishaji wa bajeti huwa zipo kwenye makundi matatu; ambayo ni ndiyo, hapana na kura zisizokuwa na uamuzi (abstain).
Wabunge wa CCM wameshangilia kwa makofi kila waliposikia “ndiyo” kutoka kwa wabunge ambao hawakuwa wametarajia kuwa wangepiga kura za namna hiyo.
Wabunge waliokuwa ndani ya Bunge kwa siku ya leo walikuwa 374 bila kumjumlisha Spika Dk Tulia (mbunge wa Mbeya Mjini) na wale ambao hawakuwa ndani ya ukumbi leo walikuwa 18.
Miongoni mwa wabunge wa CCM ambao hawakuwepo bungeni ni Dk Festo Dugange, mbunge wa Wang’ing’ombe ambaye pia ni naibu waziri wa Tamisemi, ambaye hajarejea bungeni tangu alipopata ajali Aprili 26 mwaka huu.
Kura za hapana hazikuwepo, kura ambazo hazikuwa na upande wowote zilikuwa 20 na za ndiyo zilikuwa 354 ambayo ni sawa na asilimia 95.