
Raia wa China, Wei Zhang (54) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la kukutwa na majongoo bahari yenye uzito wa kilo 4.10, ambao wapo hatarini kutoweka nchini.
Zhang ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni amefikishwa mahakamani hapo leo Juni 27, 2023 na kusomewa shtaka lake na wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Mwanga amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa kesi ya jina namba 113/2023.
Akimsomea shtaka lake, wakili Mwanga amedai mshtakiwa amelitenda Aprili 7, 2023 katika mtaa wa Kumbukumbu uliopo Kinondoni.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huku akijua jamii hiyo ya majongoo bahari ipo hatarini kutoweka, alikutwa akiwa na kilo 4.10 za majongoo bahari (Sea Cucumber) kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikana shtaka na upande wa mashtaka wamedai kuwa upelelezi umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH).
Hata hivyo, mshtakiwa aliomba apewe dhamana, ambapo Hakimu Shaidi ametoa masharti ya dhamana ambayo, mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Wadhamini hao wanatakiwa wawe na vitambulisho vya taifa pamoja na barua za utambulisho kutoka Bna watasaini bondi ya Sh 5milioni.
Baada ya kutoa masharti hayo, hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali.
Mshtakiwa amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhama.