Mwanaume ambaye hajajulikana kama ni mwanafunzi au muuguzi mkunga, anadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana wakati akifanya ngono usiku wa manane katika uchororo mjini Moshi kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Uchochoro huo uliopo mtaa wa Rengua katika Manispaa ya Moshi, unatajwa kuwa maarufu kwa ufanyaji ngono nyakati za usiku na mwaka 2020, Mwananchi iliwahi kuandika matukio yanayofanyika eneo hilo lenye urefu wa mita 60.
Uchochoro huo unaopakana na Maktaba ya mkoa na kutokea barabara ya Rengua, umezungukwa na klabu za usiku ambapo mitaa kuelekea klabu hizo hutumiwa na dadapoa kujiuza na hutumia eneo hilo kwa kufanya ngono.
Taarifa zilizopatikana juzi zilieleza tukio hilo lilitokea kati ya saa 8 na saa 9 usiku wa kuamkia jana na kwamba bado kuna utata wa kama mwanaume huyo ni mwanafunzi wa chuo kikuu kimoja jijini Dodoma au ni muuguzi mkunga.
“Nilikuwa hapa usiku wa kuamkia leo (juzi), huyo jamaa alikwenda kuchukua dada poa pale nje kwenye hiyo klabu. Huyo mwanamke akampeleka jamaa kwenye huo uchochoro,” alieleza dereva mmoja wa bodaboda.
“Sasa inavyoonekana huyo demu ana jamaa yake ni dereva bodaboda mwenzetu kwa hiyo inavyoonekana alipata wivu japo anajua demu wake anafanya shughuli hiyo ndio wakaenda wakamchoma visu wakati akiendelea kufanya ngono,” alieleza.
Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio zinadai bado kuna utata kama ni mwanafunzi au ni mwajiriwa wa Serikali kwa kuwa katika upekuzi eneo la tukio baada ya polisi kuitwa, alikutwa na vitambulisho viwili, kimoja cha mwanachuo.
“Kwa kweli polisi ndio wanaweza kusema ni mwanafunzi au mkunga muuguzi maana alikuwa na vitambulisho viwili ambavyo niliviona,” kilidokeza chanzo chetu ambacho kilisema kitambulisho cha chuo ndio kimefanya waamini ni mwanafunzi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia mauaji hayo alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wapo watu wanaoshikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
“Ni kweli usiku wa kuamkia leo (juzi) kulitokea mauaji ya kijana mmoja na tayari waliohusika na mauaji hayo tumewatambua na tunawashikilia,” alisema Kamanda Maigwa.
Aidha, Kamanda Maigwa hakutaka kusema kama kijana huyo ni mwanafunzi ama la huku akisisistiza atatoa taarifa kamili leo.