
Makamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Vincent Mwangala amesema aliyekuwa mbunge wa Mbarali, Francis Mtega alikuwa mtu wa haki na kujibidisha kwa yale yampendezayo Mungu, huku akiwaombea faraja familia yake.
Mwangala amesema hayo leo, Julai 4 wakati wa ibada takatifu ya kumuombea Mtega aliyefariki Julai 1 kwa ajali ya pikipiki alipogongwa na trekta ‘Power Tilla’ akitokea shambani kwake saa 9 mchana.
Askofu huyo amesema Mtega enzi za uhai wake alijibidisha kutii, haki na muda mwingine kulia na kubeba uchungu wa mtu mwingine na kwamba wanaiombea faraja familia yake kipindi hiki.
“Kulia na kuomboleza ni haki yetu, lakini lazima ijitofautishe na wasioamini itufikishe mahala ambapo mwenzetu ameelekea na upande huo uwe salama zaidi,” amesema na kuongeza;
“Kazi ya milele ni kumtumikia Mungu, hata mwenzetu Francis alifanya vizuri kujibidisha, alikuwa mtu wa haki mwenye kuvaa uchungu wa mtu na muda mwingine kulia kwa niaba ya wengine, upendo wake uwe shada ya kumpamba huko mbinguni,” amesema.
Mwili wa marehemu unatarajia kusafirishwa leo Jumanne kuelekea nyumbani kwao Ludewa mkoani Njombe kwa maziko kesho Jumatano.
Katika shughuli za kuuaga mwili wa marehemu vilio, simanzi na huzuni vimetawala huku mmoja wa waombolezaji akizimia wakati mwili ukiwasili kanisani.
Kitongoji cha Tazara, Kijiji cha Lyambogo na wilaya nzima ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla umeonesha kusikitishwa na kifo cha mbunge huyo.