HABARI kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa, mabosi wa timu hiyo wameamua kuwaita wachezaji wote ili kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya safari ya nje ya nchi zikitajwa Afrika Kusini au Uturuki itakapowekwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya kulingana na maelekezo ya Kocha, Roberto Oliveira.
Kundi la kwanza la wazawa lililotarajiwa kuanzia kupima jana Jumatatu, linahusisha wachezaji 12 waliopo kikosi cha sasa akiwamo nahodha John Bocco, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kibu Denis, Ally Salim, Ahmed Feruzi Teru, Israel Mwenda, Mzamiru Yasin, Jimmyson Mwanuke, Nassor Kapama, Habib Kyombo na Mohamed Mussa.
Kundi la pili litakalojumuisha wachezaji 10 wageni na kipa Aishi Manula aliyetoka kufanyiwa upasuaji hivi karibuni Afrika Kusini, litafanyiwa vipimo leo Jumanne likiwa na Moses Phiri, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Jean Baleke, Saido, Chama, Henock Inonga, Peter Banda na Pape Ousmane Sakho.
“Haya ni maandalizi ya kuanza safari ya kwenda kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya, kocha kataka wote wafanyiwe vipimo mapema kisha zianze taratibu za safari ya kwenda kuweka kambi ya msimu mpya.
“Kisha naye atajumuika wiki chache zijazo sambamba na nyota wapya walisajiliwa na watakaosajiliwa, ” alisema mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahemed Ally, alisema: “Tutatoa taarifa kamili kuhusiana na ratiba zote za timu yetu, Wanasimba wakae kwa kutulia, mambo mazuri yanakuja.”