Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, Tundu Lissu amesema mfumo na viwango vya kodi vinapaswa kuwa wazi ili anayelipa ajue analipa kiasi gani na anayekusanya ajue anakusanya kiasi gani.
Lissu ameeleza hayo leo Jumatano Julai 5, 2023 alipokutana na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na kuzungumza nao.
Amedai kilio cha wafanyabiashara wengi kinatokana na maamuzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivyo kubana haja ya kubadilisha mfumo wa ulipaji kodo.
“Haya masuala yanahitaji mabadiliko ya mifumo wa ulipaji kodi na sheria zetu za kodi, vilevile yanahitaji mabadiliko ya wakusanyaji wa kodi,”
Lisu amesema vilevile kunahitajika mabadiliko ya wakusanya kodi na kuwa na watu wenye weledi.
“Tunapaswa kubadilisha watendaji wetu wasiofaa waondolewe, watakaofaa waajiriwe, kiujumla tunahitaji watu watakaokuwa na haki,”amesema Lissu.
Lissu ametembelea soko hilo la kimataifa ikiwa ni zaidi ya mwezi upite tangu Mei 15, 2023 ambapo Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa aliongea na wafanyabiashara hao kwa mara ya kwanza baada ya mgomo wa kupinga ushuru mpya wa stoo na kero mbalimbali kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hata hivyo, Majaliwa aliagiza kusimamisha kikosi kazi cha TRA kilichokuwa kinakusanya ushuru sokoni hapo huku katika kikao chake cha pili kilichofanyika Viwanja vya Mnazi mmoja aliunda kamati ya kushughulikia kero hizo.