
Rais Samia Suluhu Hassan ametaja maeneo yanayoongoza kwa rushwa nchini kuwa ni wanasiasa, Jeshi la Polisi, ofisi za umma, Mahakama kuwa baadhi ya maeneo yanayoongoza kwa kuwa na vitendo vya rushwa, akizitaka mamlaka zinazohusika kufuatilia taasisi hizo.
Makundi mengine yanayoguswa ni pamoja na wafanyabiashara na taasisi za elimu ya juu.
Ameyasema hayo leo Julai 11, 2023 jijini Arusha katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa barani Afrika yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kusainiwa mkataba wa Umoja wa Afrika wa kupambana na rushwa.
“Rushwa inaadhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango, vitendo vya rushwa haviiishii kwenye mipaka ya kitaifa kwa kutambua hili ni muhimu kwa nchi za Afrika kushirikiana katika mapambano haya kwa kupeana misaada ya kisheria pamoja na ushirikiano wa kiufundi.
“Wala rushwa wanapaswa kufahamu kuwa nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zinazotokana na rushwa au kufuga wala rushwa, tunataka dunia nzima ifahmu kwamba Afrika si mahali salama kwa wala rushwa na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua na si mikutano, makongamano na maneno peke yake,” amesema.
Aidha amesema kuwa, Serikali inaendelea kuimarisha Taasisi ya rushwa kwa upande wa bajeti na mifumo ili kuleta ufanisi katika mapambano dhidi ya rushwa.
Ameongeza kuwa, Tanzania ilisaini mkataba huo Novemba 5, 2003 na kuridhia Febuari 22, 2005 na mkataba kuanza kutumika rasmi Agosti 5, 2006.
Amesema Tanzania ni moja ya 48 miongoni mwa nchi 55 zilizosaini na kuridhia mkataba huo.
Akizungumza awali kwenye mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Simbachawene amesema katika maadhimisho hayo mamlaka za kupambana na rushwa zilikuwa na majadiliano yaliyolenga kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mamlaka zilijitathmini namna zinavyokabiliana na rushwa na kuweka mikakati ya kuzuia rushwa, wadau pia wamepata fursa ya kubadilishana na kujadili mbinu na namna bora za kurejesha na kutaifisha mali za watuhumiwa zilizopatikana kwa njia za rushwa,” amesema Simbachawene.