
Baadhi ya wanaume wa Halmshauri ya mji Nanyamba mkoani hapa wamelalamika kunyanyaswa na wake zao wakati wakitaka unyumba kwa kupewa masharti ikiwemo kurukishwa kichurachura kuzunguka kitanda.
Akizungumza leo Julai 11 katika warsha ya viongozi wa serikali za vijiji katika halmshauri hiyo iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Smile for Community linalofadhiliwa na Legal Services Facility, Mwenyekiti wa Mtaa wa Namkuku, Andrew Mathew amesema tabia hiyo imechukuliwa ni unyanyasaji wa kingono.
“Unakuta wanaume wengine wakihitaji kupata haki zao za ndoa kuna kuwepo na mambo mengi sana yanafanyika majumbani.
“Wengine wanarukishwa kichura wanaambiwa wazunguke kitanda ili wapate haki ya ndoa, wengine wanaambiwa watoe pesa, wengine wanafulishwa nguo na wengi wanaambiwa waingie jikoni wapike na pia kuna lile kundi la kufungiwa milango na wake zao,” amesema Mathew.
Amesema manyanyaso hayo kwa wanaume yanasababisha kuwepo kwa migogoro ya ndoa, kwani baadhi ya wanaume hulazimika kutafuta wanawake wa nje ya ndoa.
“Ukikaa kuongea nao unawasikia wakielezea hii imewafanya wawe watumwa ndani ya nyumba zao, kwa hiyo wanawake wakilalamika wajue na sisi tutaanza kuvunja ukimya ili jamii ijue nini tunapitia katika ndoa zetu,” amesema.
Kwa upande wake Meneja mradi wa Haki ya Afya Kwa Maendeleo ya Binti kutoka shirika hilo, Aneth Kiyao amesema kuwa, wapo wanaume wanafanyiwa ukatili lakini hawasemi, jambo ambalo linaloifanya jamii iamini kuwa ukatili wa kijinsia ni kwa wanawake pekee.
“Ndani ya ndoa pia wapo wanawake wanabakwa na wengine wamefanywa watumwa wa ngono, ni vema tukapaza sauti kukemea haya yanayoendelea ndni ya ndoa sio sawa.
“Unawezaje kumrukisha kichurachura mumeo ili umpe haki yake ya ndoa?” amehoji Kiyao.