Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha matukio ya unyanyasaji na ukatili yanayodaiwa kufanywa na askari wa hifadhi nchini yanakoma, hali bado ni tete.
Katika maeneo mbalimbali, kilio ni malalamiko ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi kudai kunyanyaswa na kuteswa na askari wa wanyamapori wanapokuwa kwenye shughuli zao za kawaida za uzalishaji mali.
Tukio ambalo limezidisha hofu ni la mtoto wa jamii ya wafugaji Joshua Ole Patorro (15) mkazi wa Kijiji cha Nainokanoka, kudaiwa kung’olewa meno matatu na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Tukio hilo lilitokea Julai 14, mwaka huu, ambapo kabla ya askari huyo ambaye hajafahamika jina, kumfanyia ukatili mtoto huyo alipiga risasi hewani kama mbinu ya kumdhibiti.
Ilidaiwa kuwa katika tukio hilo, Patorro aliyekuwa akirejesha mifugo kutoka machungani na wenzake, mbali na kujeruhiwa, pia mbwa aliyekuwa naye alipigwa risasi.
Kutokana na tukio hilo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jeshi la Polisi pamoja na wenyeji wa Ngorongoro, wamekutana na kuunda kamati maalumu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Diwani wa Kata ya Nainokaniga, Edward Maura alilieleza Mwananchi kuwa wamekubaliana kuunda kamati hiyo na baadaye kuchukua hatua baada ya uchunguzi kukamilika.
Maura ambaye alikuwa miongoni mwa wawakilishi wa viongozi wa jamii ya wafugaji wilayani Ngorongoro walioketi kwenye kikao hicho na maofisa wa NCAA na Polisi, alisema msimamo wa wananchi ni kutaka askari aliyehusika kwenye tukio hilo la kinyama akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Tumekubaliana waunde kamati kwa ajili ya kuchunguza hili tukio, lakini msimamo wetu kama jamii ni kutaka aliyempiga mtoto na kumng’oa meno anakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Maura.
Alisema wamekuwa na makazi kwenye maeneo hayo kabla hata hifadhi hiyo kuanzishwa mwaka 1959 hivyo, wanastahiki kutendewa haki kwa kuwa wapo humo kihalali.
“Sisi sio wahamiaji haramu, tupo hapa kisheria na tumekuwa sehemu ya maisha. Sheria ya Ngorongoro ipo wazi kuwa hifadhi ilianzishwa kusaidia utalii, kuendeleza uhifadhi na kuendeleza jamii inayoishi humu na wakati inaanzishwa tayari tulikuwa sehemu ya wakazi,” alisema Maura.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Elibariki Bajuta alisema wameanza uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kuwabaini waliohusika na chanzo chake.
“Tumeanza kufanya uchunguzi kujua tatizo na baadaye tutatoa taarifa,” alisema Bajuta.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nainokanoka, Lenyori Lemayani na kiongozi wa kimila wa Kimasai, Laigwanani Kisika Kiloriti, walisema pamoja na kuridhia kuundwa kwa kamati hiyo, kikubwa wanachotaka ni kukomeshwa kwa matukio ya kikatili na unyanyasaji dhidi ya wananchi.
Lemayani alisema katika siku za karibuni kumekuwa na matukio ya wafugaji kukamatwa na kupigwa wanapokuwa machungani jambo ambalo hawakubaliani nalo.
Aliyataja maeneo kinara kwa matukio hayo kuwa ni Olmoti na Embakai ambayo kwa sasa ndio kimbilio lao kutokana na kuwa na maji kwa ajili ya mifugo yao.
“Olmoti na Embakai kwa sasa ndio maeneo yenye maji ambayo tunaweza kupeleka mifugo yetu, sasa wanapotuzuia hatufahamu wapi twende kupata maji,” alisema.
Laigwanani Kiloriti, kwa upande wake, alisema kwa sasa kuna viashiria vya kutokuwepo kwa amani na uhusiano mzuri baina ya hifadhi na wananchi na ugomvi unaoendelea utaleta tafrani kubwa. “Nataka amani irejeshwe, sisi tumeamua kuishi Ngorongoro kwa hiari yetu na hatuwezi kamwe kuhama kama wengine,” alisema.
Hadi kufikia Januari, mwaka huu kaya 523 zenye watu 2,808 na mifugo 14,757 zilikuwa zimeshahama kutoka tarafa ya Ngorongoro kuhamia kwa hiari Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Msomera na maeneo mengine yameandaliwa kwa ajili ya mkakati wa Serikali kupunguza idadi ya wananchi walioweka makazi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, ili kulinda eneo hilo dhidi ya uharibifu mkubwa wa mazingira hivyo, kuwa kwenye hatari ya kutoweka.
Mama wa mtoto ataka sheria
Mama wa mtoto anayedaiwa kufanyiwa ukatili huo wa kung’olewa meno, Nanja Partoro, aliomba sheria ichukue mkondo wake ili kupoza maumivu ya mwanawe ambaye hana baba.
“Ninaomba aliyefanya ukatili kwa mwanangu akamatwe na afikishwe mahakamani, najua Serikali itamkamata askari aliyempiga na kumng’oa meno,” alisema.
Naye Lanyor Kuya ambaye amekuwa akimuugiza Partoro katika Hospitali ya Double D iliyopo Karatu, alidai alipigwa na askari akiwa anatoka kuchunga eneo la Olmoti akiwa na wenzake.
Alidai kutokana na kipigo hicho, Partoro alizimia na aliokotwa na marafiki zake, ambao awali walifanikiwa kukimbia baada ya askari wa hifadhi kupiga risasi juu na kumpiga risasi mbwa waliyekuwa naye.
Vurugu Mbarali
Mei 6, mwaka huu wananchi watano katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya walilalamikia kujeruhiwa na Askari wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (Tanapa).
Kutokana na tukio hilo, Mei 11 mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Mbarali (CCM), marehemu Francis Mtega aliomba Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili tukio hilo la madai ya kuumizwa kwa wananchi, kuua mifugo na kupora mifugo. Wakati mbunge huyo akitoa kilio chake bungeni, siku mbili baadaye Serikali ilikanusha madai hayo.
Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hili alitembelea kijiji hicho na kuzungumza na wananchi waliokiri kupigwa, kushambuliwa huku wakisimulia tukio lilivyokuwa na kuonyesha majeraha.
Mei 15, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa alilieleza Bunge kuwa hakukuwa na uporaji mifugo, watu kuumizwa wala mbuzi waliouawa kwa risasi kutokana na vurugu hizo.