KIONGOZI wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko, ambaye amekuwa akisusia chakula wakati akiwa gerezani kama njia ya kulalamikia mashitaka ya jinai dhidi yake, Jumapili amelazwa hospitalini, kulingana na ripoti kutoka chama chake.
Sonko alipelekwa jela wiki iliyopita kabla ya kesi yake kusikilizwa, akituhumiwa kuitisha mapinduzi dhidi ya serikali miongoni mwa mashitaka mengine. Kwa mujibu wa shirika la habari la AP sababu hasa ya Sonko ya kulazwa kwenye hospitali kuu mjini Dakar haijatolewa, ingawa alikuwa buheri wa afya bila kuwa na maradhi yoyote yanayojulikana kabla ya kuwekwa jela, chama chake kilichopigwa marufuku cha Patriots of Senegal kimesema.
Hapo Julai 30, Sonko kupitia ukurasa wake wa Twitter ambayo sasa inafahamika kama X alisema kwamba angeanza kususia chakula. Tangazo hilo lilikuja siku moja tu kabla ya jaji wa mahakama ya Dakar kuamuru apelekwe jela. Mashitaka ya karibuni dhidi ya Sonko yamekuja wiki chache baada jaji kumpata na hatia ya kuchochea vijana na kutoa hukumu ya miaka 2 jela, hatua iliyosababisha maandamano makali kote nchini.
Wiki iliyopita, takriban watu wanne walikufa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa kwenye maandamano mapya baada ya Sonko kupelekwa jela iliyoko nje kidogo ya mji mkuu, wa Dakar. Taarifa za hali ya afya ya Sonko zimekuja siku moja baada ya wakili wake Juan Branco kukamatwa akiwa Mauritania na kisha kurejeshwa Senegal ambako amezuliwa kwenye jela moja mjini Dakar, kulingana na wakili wake Robin Bindard. Sonko alishika nafasi ya 3 kwenye uchaguzi wa rais wa 2019, wakati akiwa na umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.