
Uamuzi wa kesi ya kupinga mkataba wa ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii,kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA), unaohusu uwekezaji katika Bandari za baharini na katika maziwa Tanzania, uliokuwa umepangwa kutolewa leo, Jumatatu, Agosti 7, 2023, umeahirishwa.
Uamuzi huo ulikuwa umepangwa kutolewa leo asubuhi hii na jopo la majaji watatu walioisikiliza kesi hiyo, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya; linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.
Hata hivyo umeahirishwa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo Projest Kahyoza kwa siku tatu zaidi mpaka Alhamisi Agosti 10 mwaka huu, kutokana na mwenyekiti wa jopo la majaji kuwa na dharura.
“Kweli uamuzi huu ulikuwa umepangwa kutolewa leo kama mawakili walivyoeleza.”, amesema Naibu Msajili baada ya mawakili wa pande zote kujitambulisha na kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa leo Kwa ajili ya uamuzi na kwamba wako tayari kuupokea, kisha akaendelea:
“Kwa bahati mbaya mwenyekiti wa jopo amepata dharura hayupo, kwa mambo ambayo hayazuiliki. Kwa hiyo wamekubaliana kwamba mpaka wote wawezo. Kwa hiyo ameelekeza maamuzi haya yasomwe Alhamisi ya wiki hii, tarehe 10, 2023.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na mawakili wanne kutoka mikoa tofautofauti, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshahri wa Serikali kwa mauslanya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.
Katika hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023, wanasheria hao vijana wanapinga makubaliano hayo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya Ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.
Vile vile wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.
Makubaliano hayo yalisainiwa Oktoba 25, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, baada ya kupewa nguvu ya kisheria na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, akishuhudia na yaliridhiwa na Bunge Juni 10, 2023.