Mshindi wa pili katika uchaguzi wa rais wa Zimbabwe, Nelson Chamisa, amedai kushinda baada ya kukataa matokeo rasmi ambayo yalimtangaza aliyemaliza muda wake Emmerson Mnangagwa mshindi kwa karibu asilimia hamsini na tatu ya kura.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi huo, Chamisa alimshutumu mpinzani wake kwa kuandaa mapinduzi ya uchaguzi.
Wakati huo huo Mnangagwa aliwashukuru Wazimbabwe kwa kupiga kura, akikana shutuma kwamba kura hiyo haikuwa ya haki au ya uwazi.
Nelson Chamisa wa chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change alipata asilimia 44 ya kura.
Katika mkutano na wanahabari alishutumu Tume ya Uchaguzi kwa kutangaza matokeo ya uongo, lakini bado hajatoa ushahidi.
Waangalizi wa kimataifa pia walikosoa uchaguzi huo. Chama tawala cha Zanu PF kimeutaka upinzani kupeleka mzozo wowote mahakamani.
Bw Chamisa ana wiki moja kufanya hivyo lakini hakusema iwapo chama chake kitachukua mkondo huo wa kisheria.