Katibu mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ameikabidhi timu ya Twiga Stars shilingi Milioni 10 zilizotelewa na Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia ushindi walioupata dhidi ya Ivory Coast.
Msigwa amesema wachezaji hao wanafanya kazi kubwa ya kuiwakilisha nchi kimataifa na Seriakali ipo pamoja nao kwa kuwa wanaitangaza na kuipigania nchi yao.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapongeza sana, anafurahi sana anapowaona mnacheza uwanjani, anafurahi sana mnapopata matokeo mazuri katika mechi zetu.” Amesema Msigwa
Kwa upande wake kocha mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime amesema, amefurahi kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rais Samia na kwamba fedha hizo zitawahamasisha wachezaji hao kujituma zaidi.
Naye nahodha wa Twiga Stars, Joyce Lema amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuzidi kuwapa hamasa na kumuahidi kutomuangusha katika mashindano yote yaliyo mbele yao.