Rais William Ruto wa Kenya Jumanne aliziagiza wizara kupunguza bajeti zao za mwaka 2023/2024 kwa asilimia 10 ili kuoanisha matumizi na rasilimali zilizopo kufuatia matatizo ya kiuchumi duniani.
Ruto pia alisisitiza haja ya serikali kutumia busara katika matumizi ya rasilimali, akisema kwa uthabiti kwamba ufujaji na ufisadi hautavumiliwa.
Ikulu ya rais ilisema kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi baada ya mkutano wa baraza la mawaziri kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya bei, serikali itatenga shilingi bilioni 4 za Kenya, sawa na dola milioni 26.96 za Kimarekani kununua mahindi kutoka kwa wakulima.
Hatua hii mpya ilikuja siku moja baada ya serikali ya Kenya kusimamisha safari zisizo muhimu kwa maafisa wa serikali huku ikijaribu kupunguza matumizi na kuhakikisha matumizi ya fedha yanakuwa na busara.