Waziri Mkuu Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wawafuatilie na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 waliokuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili wajibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Oktoba 3, 2023) kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo.
“Watumishi wa Jiji la Dodoma ni Josephat Mafuru (aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji), Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Agusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi. Hawa ni wachache miongoni mwa wengi waliohusika kusababisha migogoro, watafutwe na waje kujibu tuhuma dhidi yao,” amesema.