AHMED Ally, Meneja wa idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa mchezo wao dhidi ya Mashujaa FC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex utakuwa mgumu kulingana na wapinzani wao kuwa bora.
Mchezo huo ni kiporo ratiba yake imepangwa upya kwa kuwa Simba SC ilikuwa kwenye mechi za kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa imetinga hatua ya fainali na inatarajiwa kucheza na RS Berkane.
Simba SC kutoka Tanzania itaanzia ugenini kwenye fainali yake ya kwanza inayotarajiwa kuchezwa Mei 17 na fainali ya pili inatarajiwa kuchezwa Mei 25 Dar itakayotoa mshindi wa jumla atakayetwaa taji hilo la Afrika.
Ally amesema kuwa kila mchezo wanauchukulia kwa umuhimu na wanatambua hakukuna kazi nyepesi hivyo watapambana kupata matokeo chanya ndani ya uwanja.
“Hakuna mchezo mwepesi kwetu na tunatambua kwamba wapinzani wetu Mashujaa FC wapo imara hivyo hatuwabezi tunawaheshimu kuelekea mchezo wetu muhimu na ambacho tunahitaji ni pointi tatu.
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuongeza nguvu kwa wachezaji kwa kuwa uwepo wao ni muhimu na silaha yetu kubwa kupata matokeo kwenye mechi zetu zote huwa inakuwa kwa shabiki ambaye ni mchezaji wa 12.”
Novemba Mosi 2024 kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganika baada ya dakika 90 ubao ulisoma Mashujaa 0-1 Simba SC, hivyo Mashujaa wataingia uwanjani kusaka kisasi na Simba SC kulinda rekodi.
Steven Mukwala ambaye alianzia benchi kwenye mchezo huo alipachika bao la ushindi dakika ya 90 akitumia pasi ya Awesu Awesu ambaye naye alianzia benchi katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Simba SC ilikomba pointi tatu ugenini inatarajiwa kukutana na Mashujaa, Mei 2 2025 Uwanja wa KMC Complex ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa pili kwa wababe hawa kukutana ndani ya uwanja katika msako wa pointi tatu muhimu.