
Katika mchakato wa awali wa kuchuja majina ya watia nia wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Mrisho Gambo, amejikuta akikosa nafasi ya kuingia kwenye tatu bora zilizopitishwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya.
Licha ya kuwa mmoja wa wagombea waliovuta hisia kubwa kwa wanachama na jamii, jina la Gambo halikupenya kwenye hatua ya kwanza ya mchujo huo, hali inayoibua taswira mpya ya ushindani ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tatu bora waliopitishwa katika hatua hii ya awali wataendelea kuhiojiwa kwenye ngazi ya Mkoa, kisha Taifa, kabla ya jina la mgombea mmoja kurudishwa kwa wajumbe wa chama ili kupigiwa kura na hatimaye kuteuliwa rasmi kuwa mgombea wa CCM katika jimbo hilo nyeti.
Hata hivyo, mchakato bado unaendelea, na hakuna kinachofungwa rasmi hadi chama kitakapotoa orodha ya mwisho ya majina kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao. Macho sasa yanaelekezwa kwenye hatua za juu za mchujo, huku majina mengine yakitajwa kuibuka na ushindani ukiwa mkali zaidi.
