BAADA ya taarifa za Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole kujiuzulu nafasi ya Ubalozi nchini Cuba zimeshtua wengi na kuwafanya wapigwe na butwaa huku wakijiuliza kulikoni, miongoni mwa walishtuliwa zaidi ni kada mwenzake, Comredi Khamis Mgeja ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga ambaye kwa sasa yupo nchini India kwa matibabu.
Taarifa za Polepole kujiuzulu nafasi hiyo kwa kudai kupinga mwenendo wa chama chake zilianza kuzagaa juzi, Julai 13 siku ya Jumapili ambapo awali wengi walionesha kutoamini na kusema huenda kuna waharifu wamedukua mitandao yake na kumzushia taarifa za uongo (Fake news).
Lakini kadili muda ulivyokwenda hatimaye ulimwengu ukaanza kuamini taarifa hizo zilizozagaa kupitia mtandao wake wa instagramu huku mwenye bila kuonekana kukanusha popote kuhusu taarifa hizo.
Kufuatia hali hiyo miongoni mwa waliojitokeza kuonesha kusikitishwa na hali hiyo ni kada wa muda mrefu wa chama hicho, Khamis Mgeja ambaye amewahi kushika nasi mbalimbali za uongozi wa juu wa chama hicho mkoani Mwanza.
Mwenyekiti huyo Mstaafu Mgeja akizungumza na mwanahabari wetu kutokea nchini India amesema miongoni mwa kinachomshangaza ni Polepole kufanya hayo kipindi hiki ambacho chama kikiwa kwenye harakati za uchaguzi mkuu.
Ameelezea madhara ya jambo kama hilo hususan kipindi hiki ni pamoja na kuwaondolea imani wengine wenye imani na CCM na hivyo kukiyumbisha chama na kukiingiza hatarini. Amesema Mgeja.
“Kama yeye anaona chama hakifai basi ni bora angejiweka hadharani kuwa anahamia chama kingine ili akaendeleze harakati zake huko kama wenzake wakaki kukutana majukwaani tofauti na anavyokidhalilisha chama huku anasema ataendelea kuwa mwana CCM mtiifu.
“Namshauri Polepole kukumbuka heshima aliyowahi kupewa na chama hicho kuwa ni pamoja na kuteuliwa nafasi mbalimbali kama vile Katibu Mwenezi, Mkuu wa Wilaya, Mbunge wa Kuteuliwa pamoja na nafasi hiyo ya ubalozi aliyotangaza kujiuzulu”. Alimaliza kusema Mgeja.