Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa makombora ya kisasa ya kujihami ya Patriot tayari yamepelekwa nchini Ukraine chini ya mpango mpya wa utoaji unaohusisha ushirikiano kati ya Marekani, NATO na Umoja wa Ulaya.
Trump aliyasema hayo Jumanne wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, ambapo alikata kauli ya mwandishi aliyekuwa anauliza kuhusu mpango huo wa misaada ya kijeshi kwa Ukraine na kueleza moja kwa moja:
“Tayari wametumwa,” alisema Trump kwa msisitizo.
“Yanatoka Ujerumani na Ujerumani itayabadilisha. Na katika hali zote, Marekani italipwa kikamilifu.”
Akiweka wazi zaidi mpango huo, Trump alieleza kuwa mfumo wa utoaji wa silaha hizo unahusisha mataifa washirika wa NATO na Umoja wa Ulaya, lakini akasisitiza kuwa Marekani haitabeba mzigo wa gharama pekee.
“Kimsingi ni Umoja wa Ulaya unayatoa, lakini wacha tuseme kwa njia ya NATO, ni sawa sana. Lakini NATO itatulipa kwa kila kitu. Katika baadhi ya matukio, tutalipwa moja kwa moja na nchi za Umoja wa Ulaya,” aliongeza.
Vikwazo kwa Mafuta ya Urusi
Katika mahojiano hayo, Trump pia aligusia suala la vikwazo vya pili kwa nchi zinazonunua mafuta kutoka Urusi, suala linalozua mjadala mkubwa wa kimataifa kuhusu athari zake kiuchumi.
Alipoulizwa kama vikwazo hivyo vinaweza kuwaumiza watumiaji wa kawaida wa Marekani, Trump alisema:
“Sidhani hivyo. Nadhani jambo hili lote litaisha mwishowe. Linapaswa kuondolewa.”
Akaongeza kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameonyesha dalili za kutaka kumaliza mgogoro huo, lakini bado hajachukua hatua thabiti.
“Putin anasema, ‘Nataka amani, nataka amani,’ lakini bado hajafanya kile anachosema. Kwa hivyo nadhani litaondolewa. Lakini tutaona.”