NAHODHA wa Simba SC, Mohamed Hussen Zimbwe Jr kuna hatihati huenda akaondoka ndani ya kikosi hicho baada ya kanadarasi yake kugota mwisho msimu wa 2024/25.
Zimbwe kwenye ukurasa wake rasmi wa Instgarm ameondoa utambulisho wake kuwa ni mchezaji wa Simba SC. Ipo wazi kwamba kwa sasa yupo huru akiwa hajaongeza mkataba na mabosi wake hao kwa msimu wa 2024/25.
Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Yanga SC wanafanya mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo huku Simba SC nao wakiwa kwenye mazungumzo na mchezaji huyo kumpa mkataba mpya.
Ikumbukwe kwamba kwa msimu wa 2024/25 Zimbwe Jr alicheza jumla ya mechi 27 kati ya 30. Alikosekana kwenye mechi tatu pekee akiwa ni chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Beki huyo alikomba dakika 1,817, alihusika kwenye mabao manne kati ya 69 yaliyofungwa na timu hiyo. Alifunga bao moja akitoa pasi tatu za mabao.
Hivi karibuni, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally aliweka wazi kuwa kuna wachezaji ambao mikata yao imeisha na wapo ambao bado wana mikataba ila kuna timu ambazo zinawahitaji.
“Kuna wachezaji ambao mikataba yao inaisha na wapo wengine ambao bado mikataba inaendelea lakini kuna timu ambazo zinawahitaji hivyo ni muda wakusubira na Wanasimba wawe na subira.”