Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi ameendelea kuwa faraja kwa wananchi wa Wilaya hiyo baada ya kumtua kilio mzee mmoja aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume na uvimbe kwa zaidi ya miaka miwili na kushindwa kumudu gharama za matibabu hivyo ataanza kupata huduma ya matibabu Agosti 7 mwaka huu katika Hospitali ya Dr. Jakaya Kikwete Kishapu.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa Mhunze uliofanyika Kitongoji cha Mwasele “B” Mhunze, ambapo wananchi wamepata elimu juu ya fursa za mikopo ya Halmashauri, biashara, utaratibu wa kupata vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na huduma za benki, Mhe. Masindi ametumia fursa hiyo kuhimiza wananchi kutambua thamani ya muda na kujikita katika shughuli zenye tija.
“Vipo vitu vitatu ambavyo ni mhimili mkubwa kwa mwanadamu kwanza ni kujali muda, kumpenda Mungu, na pia kujali watu. Mbali na hayo, hakuna maendeleo yatakayompata mtu asiyezingatia hayo,” amesema Mhe. Masindi huku akipongeza jitihada za baadhi ya wananchi walioanza kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.
Aidha, DC Masindi amewataka wananchi wa Kishapu kuacha kupoteza muda kwa mambo yasiyo na faida na badala yake wafanye kazi kwa bidii na kuweka akiba ili kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Afisa Biashara wa Wilaya ya Kishapu, Ezekiel Alphonce, ameeleza kuwa Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 100 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kuboresha vibanda vya mnada wa Mhunze huku maboresho hayo yakijumuisha ujenzi wa vibanda vya kisasa vya biashara pamoja na vyoo vya matundu matatu katika eneo la maegesho ya magari.
Mzee Lameck Kiyaga, amempongeza Mkuu huyo kwa kutenga muda wake kusikiliza kero mbalimbali za wananchi ameongeza kwa kuombauboreshaji wa vibanda vya kisasa kwenye Mnada wa Mhunze yaambatane na uwepo wa huduma ya miundombinu ya maji, umeme na mazingira bora kwa wafanyabiashara.
Kwa upande mwingine, Mhe. Masindi amevitaka vikundi vyote vinavyodaiwa fedha na Halmashauri kuhakikisha kuwa vinamaliza madeni yao ifikapo Novemba 6, 2025 akisema kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa vikundi vitakavyokaidi agizo hilo.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kuwa na uthubutu wa kuanzisha biashara na kutumia fursa zilizopo katika mnada wa Mhunze kwa maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Katika Mkutano huo Mhe Masindi amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kishapu kujitokeza kwa wingi kupokea Mwenge wa Uhuru utakaoingia Agosti 8,2025 ukitokea Manispaa ya Shinyanga kuunga juhudi za serikali ya awamu ya sita huku Mwenge huo wa Uhuru ukikagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ikiwemo Kilimo,Elimu,Maji,Afya,Barabara uwekezaji Wilayani humo.